BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirikisho
la Sanaa za Ufundi nchini liko mbioni kuzindua kampeni itakayolenga
kujenga msukumo wa kulipamba taifa na sanaa mbalimbali nyumbani.
Akizungumza wiki hii kwenye kikao cha awali cha maandalizi ya kampeni
hiyo kilichofanyika makao makuu ya BASATA Ilala Sharifu Shamba jijini
Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa baraza hilo Ghonche Materego alisema
kuwa, lengo ni kuhakikisha maeneo ya miji, majiji, manispaa, ofisi,
mahoteli na mazingira mbalimbali yanaona umuhimu wa kununua sanaa za
nyumbani na kuzitumia kupamba.
“Hatujapamba kabisa kwa sanaa zetu, maeneo mengi ya miji, kuta za
maofisi, nyumba zetu na kadhalika ni matupu. Ni wazi kunahitajika
msukumo wa kipekee katika kuhakikisha tunaipendezesha nchi yetu kila
mahali kwa kutumia sanaa zetu mbalimbali,” alisisitiza Materego.
Alisema inasikitisha kuona Tanzania ikiwa ni nchi iliyojaliwa vipaji
vingi na yenye historia ya pekee katika Sanaa za Ufundi haijatumia
mapambo ya sanaa kama ilivyotarajiwa.
“Inatakiwa kuta za nyumba, maeneo ya wazi, pamoja na majengo mbali
mbali yapambwe kwa kazi zetu za sanaa, ni ajabu kuona miji mbali mbali
haijapambwa mtu unatembelea, fukwe, maofisi, shule, majumba, mahoteli na
maeneo mengine lakini unakuta yamepambwa kwa kuigiza Umagharibi,”
alisema Materego.
Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete kwa
kutilia mkazo mapambo ya sanaa za nyumbani na kutoa wito kwa ofisi
nyingine za umma kuiga mkakati huo kwani ni aibu kutumia sanaa za nje
kupamba.
Alisema nchi ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayovuma kwa sanaa
za ufundi duniani kama: Michoro, vinyago, ususi na kadhalika lakini
pamoja na utajiri huo bado sanaa hizi hazijathaminiwa nchini.
No comments:
Post a Comment