Wema Sepetu.
Shakoor Jongo na Musa MatejaWASWAHILI husema ‘penzi ni kikohozi, kulificha huwezi’, usemi huo ulidhihirika Juni 15, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Golden Tulip jijini Dar ambapo kulikuwa na shindano la kumpata Miss Dar City Centre wa mwaka 2012/13.
Katika shindano hilo, staa wa Muziki wa Bongo Fleva anayeng’aa vizuri kwa sasa, Naseeb Abdul ‘Diamond’ alijikuta akilazimishwa na nguvu ya umma kujirudi kwa mchumba wake wake wa zamani, Wema Isaac Sepetu.
ISHU ILIANZA HIVI
Wakishuhudia tukio la ‘Platinumz’ kujirudi kwa Wema, wapiganaji wa Ijumaa Wikienda walimsikia msanii huyo akipindisha kwa makusudi mashairi ya wimbo wake wa Nimpende Nani? akianza kumsifia Wema Sepetu huku akimaanisha kuwa anachoimba anakifahamu na kutaja cheo ambacho mrembo huyo alikuwa nacho usiku huo, cha ujaji.
WIMBO HALISI UKO HIVI:
“…yasiwe kama ya Wema Sepetu, kila siku magazeti,
ajue nidhamu na mila ya kwetu, mjuzi kupeti-peti,
simtaki ka’ Uwoya ni mtemi ana hasira, mpole kama Jokate, ila sauti ka’ Wema akiwa analia, kicheko kama cha Fetty…”
WIMBO WA UKUMBINI ULIKUWA HIVI:
“…asiwe kama Jaji Sepetu kila siku magazeti, ajue nidhamu na mila ya kwetu, mjuzi kupetipeti, simtaki ka’ Uwoya ni mtemi ana hasira, mpole kama … (akakaa kimya na kuacha mashabiki wakimalizia kwa kusema, Wemaaa).”
Diamond akaendelea: “Ila sauti kama ya Jaji Sepetu akiwa analia, mpole kama … (akakaa kimya kwa mara nyingine na kuwaacha mashabiki wamalizie ambapo walisema kwa sauti za juu, Wemaaaaa.”
Akiendelea kubadili mashairi ya wimbo wake huo, Diamond alidiriki kuacha baadhi ya majina ya warembo wengine aliowataja, Jokate na Fetty na kuingiza vipande ambavyo viliashiria kumwangukia mrembo huyo.
MKUU WA WILAYA TEMEKE AUNGA MKONO
Tukio jingine la kufurahisha ambalo liliandika historia ya aina yake ni pale Diamond alipouliza mashabiki wake kwa kutumia ‘maiki’, Nimpende Nani? ambapo Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bi. Sophia Mjema aliungana na mashabiki kujibu: “Wemaaa.”
UMATI WALIPUKA KWA FURAHA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, umati wa watu ukumbini humo ulilipuka kwa furaha baada ya kumsikia Diamond akimsifia Wema mara kwa mara tofauti na siku ile ya shoo yake ya Mlimani City, iliyojulikana kwa jina la Diamond Are Forever ambapo wawili hao walitibuana kufuatia kitendo cha msanii huyo kupotezea fedha za kutuzwa kutoka kwa Wema.
“Nimefarijika sana kuona Diamond anaanza kujirudi taratibu kwa Wema kwani ndiyo ‘saizi’ yake, wanaendana kabisa,” alisikika shabiki mmoja aliyekaa jirani na meza ya wageni rasmi.
JOKATE AINGIA MITINI
Hata hivyo, katika hatua nyingine, Miss Tz No. 2, 2006, Jokate Mwegelo ambaye kwa sasa ndiye mpenzi wa Diamond, alidaiwa kutofika kwenye shindano hilo baada ya kupigwa mkwara na shoga yake kipenzi sanjari na Diamond mwenyewe.
Habari zinadai kuwa, wawili hao walimpiga biti Jokate ambaye aling’anga’nia kutia timu wakimkumbusha hali ilivyokuwa siku ya kumsaka Miss IFM, 2012 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar ambapo Jokate na Wema nusura wazichape baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yao.
“Unajua hakuna kitu kizuri kama kumbukumbu. Katika shindano la kumsaka Miss IFM pale Ubungo Plaza tulikaa meza moja na Wema lakini kilichotokea ndiyo vile tena, Jokate alitofautiana na Wema, akazomewa kiasi kwamba alishindwa hata kwenda chooni. Ndiyo maana leo nikamwambia asije hapa, nikamkumbushia yaliyotokea Ubungo Plaza,” shosti wake alimwambia paparazi wetu.
WEMA SITAKI NATAKA, KISHA MENO NJE
Awali, Wema alikaririwa na paparazi wetu akisema kuwa japo ni jaji wa shindano hilo, Diamond atakapopanda jukwaani hatainua uso wake kumwangalia mpaka anashuka kwa sababu akikumbuka mambo aliyomfanyia anajisikia vibaya.
Hilo lilitimia kweli, kwani Diamond alipopanda jukwani na kuanza kuimba wimbo wake wa kwanza, Wema alikuwa bize na simu. Hata alipoimba wimbo wa pili, hali ilikuwa sawa na kiapo chake.
Hata hivyo, alipoimba wimbo wa tatu Nimpende Nani na kuingiza maneno ya kumchombeza huku mashabiki wakisema Wema, supastaa huyo alianza kutabasamu chini kwa chini, mwishowe aliinua uso na kumtazama msanii huyo kwa macho yenye furaha huku akicheka.
NYUMA YA PAZIA
Habari zinadai kuwa, Diamond alilazimika kuingiza mashairi yenye kumsifia Wema ili kumaliza bifu lao ambapo inasemekana kuwa tangu shoo ya Diamond Are Forever, pale Mlimani City, wawili hao hawakuwahi kukutana ‘laivu’.
DIAMOND ANA CHA KUSEMA?
Baada ya shindano hilo, Diamond, akizungumza na gazeti hili hakutaka kufafanua madai ya kutumia mashairi yenye kumrembaremba Wema ili kujirudi dhidi ya bifu lao, lakini alikiri kumwambia Jokate asifike kwenye shoo hiyo ingawa hakuweka wazi sababu.
WALIOIBUKA WASHINDI MISS DAR CITY CENTRE
Shindano hilo liliisha kwa mshiriki Matilda Martin kutwaa Taji la Miss Dar City Centre, 2012 huku Magdalena Raymond akinyakua nafasi ya pili na Witness Michael kukalia namba tatu.
No comments:
Post a Comment