
Na Saleh Ally, Maputo
SIKU chache baada ya kusaini kuichezea Yanga, kiungo kinda, Frank Raymond Domayo, amepata bahati ya kuonekana na huenda akafanya majaribio katika Klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno.
Sporting Lisbon ndiyo timu iliyomkuza kisoka mshambuliaji nyota wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, aliyezaliwa katika kisiwa cha Madeira.
Akizungumza juzi usiku mjini hapa, wakala maarufu wa kuuza wachezaji kutoka Afrika, Fransico Diogo, alisema amevutiwa na Domayo na tayari amezungumza na klabu hiyo.
“Nilikuwa Angola, nimekuja hapa (Maputo) kwa ajili ya kuwaangalia wachezaji wawili wa Msumbiji, lakini nimemuona huyu namba 16 (Domayo). Ni mchezaji bora na ni kijana.
“Tayari nimefanya mawasiliano na Sporting Lisbon, nataka kujua kama watakuwa tayari kumchukua. Nimewaambia hajawa tayari lakini anaweza kukuzwa na baadaye akafanya vizuri.
“Nitawasiliana na timu yake mara moja baada ya kupata jibu, kocha wake pia ameniambia bado ni mchezaji mdogo sana,” alisema Diogo.
Wakala huyo alisema anarejea nchini Angola ambako awali alikuwa amekwenda kusaini mikataba na klabu mbili nchini humo kwa ajili ya kuwatafutia timu wachezaji wa klabu hizo.
Kama atakuwa amepata jibu, huenda akawaomba Yanga ili Domayo aende Ureno na kama itashindikana, atatuma video za mechi ya Msumbiji dhidi ya Taifa Stars ili kujua kama wako tayari kumchukua na mazungumzo na Yanga yaanze mara moja.
Domayo amejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea, JKT Ruvu.
Katika mechi hiyo ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Kilimanjaro, Domayo alionyesha uwezo mkubwa na wakati fulani kwa kushirikiana na Haruna Moshi ‘Boban’, Kelvin Yondani na Shabani Nditi, waliwalazimisha mashabiki wa Msumbiji kuizomea timu yao baada ya kugonga zaidi ya pasi 22 bila ya wenyeji kugusa mpira.
Diogo pia alivutiwa na mshambuliaji kinda, Thomas Ulimwengu ambaye alicheza kwa dakika 45 na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Moshi ‘Boban’.
No comments:
Post a Comment