Na Mwandishi Wetu, Simiyu
AMA kweli ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Firauni! Msemo huu unakwenda sambamba na tukio la hivi karibuni la mkazi mmoja wa Kijiji cha Nghoboko wilayani Meatu mkoani hapa, Stephano Mihilu mwenye miaka 60, kudaiwa kumfumania mkewe wa ndoa akifanya mapenzi na mtoto wao wa kumzaa.
Taarifa za kipolisi zilizotua kwenye dawati la Amani zinadai kuwa tukio hilo la aina yake lilitokea usiku wa Julai 22, mwaka huu ambapo baada Stephano kulishuhudia tukio hilo, aliwaua mama na mwanaye kwa kuwacharanga mapanga bila huruma.
“Jamaa aliporudi nyumbani, aliingia ndani na kukutana na tukio ambalo hakuwahi kulifikiria, alimkuta mkewe akifanya mapenzi na mtoto wao wa kumzaa, nadhani akili ilihama, akachukua panga na kuwacharanga wote mpaka walipokata roho,” alisema afande mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwani si msemaji wa jeshi la polisi.
HUYU HAPA KAMANDA WA POLISI WA SIMIYU
Akilizungumzia tukio hilo la kusikitisha na kushangaza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Afande Salum Msangi aliwataja waliouawa kuwa ni Kundi Sita mwenye umri wa miaka 40, ambaye alikuwa mkewe na Boyani Stephano mwenye miaka 27 ambaye ni mtoto wao wa kumzaa.
Alidai kuwa, Mihilu alimkuta mkewe akifanya tendo la ndoa na mtoto wake wa kumzaa ndipo alipopandwa na hasira kisha kuwashambulia kwa kuwakata mapanga na baadaye kuwachinja.
Kamanda Salum alisema, baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alikwenda mwenyewe kujisalimisha kwenye kituo cha polisi ambapo alikabidhi silaha alizotumia katika mauaji hayo ambazo ni panga na fimbo.
“Mihilu alitembea kuanzia saa 7 usiku hadi asubuhi kwenda katika Kituo cha Polisi cha Mwahuzi wilayani Meatu kwa lengo la kujisalimisha akidai kuwa hakutaka kuwasumbua wanausalama hao kwani yeye ndiye mhusika wa mauaji hayo,” alisema kamanda huyo.
WANANCHI WANALIZUNGUMZIAJE TUKIO HILO?
Wakizungumza na mwandishi wetu baada ya tukio hilo, baadhi ya wananchi wameonesha kushangazwa nalo huku wakieleza kuwa, kama ni kweli basi dunia inaelekea mwisho.
“Hivi inawezekanaje mama kufanya tendo la ndoa na mwanaye wa kumzaa? Au kuna mazingira ya ushirikina?” alihoji Juma Sagala wa Meatu.
Naye Mama Josephine, mkazi wa kijiji ambacho tukio hilo lilitokea alisema: “Hili tukio lina utata lakini kwa kuwa limeshafika kwenye vyombo vya dola, ukweli utajulikana na sheria itachukua mkondo wake ila limetushangaza sana.”
No comments:
Post a Comment