Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 30 JUNI, 2012
Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu
mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya
kwanza ya mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza
nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo
la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili
ni la mgomo wa madaktari.
Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43
za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha
Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja
na maiti hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa
wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa
kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi
walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine
walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha
kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi
na baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda
kuishi Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza
miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne
waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori
na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego. Lori
walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa
kukosa hewa.
Tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine
kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika
kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la
wahamiaji haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi
sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500
tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi
wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na
Bangladesh.
Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo
rasmi. Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za
Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani
Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji
nchini kuhamia bali wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini
ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na
Ulaya. Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum
wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia
mpaka kule waendako. Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili
wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si
suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha
binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa
ndipo wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo.
Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji
yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo. Usafiri wa aina hiyo ndiyo
uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara
hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa
pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli
za biashara hii haramu hapa nchini. Tulielewana kuwa waendelee
kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006
kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili
tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane
na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini
kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari nimeshaanza
kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu ushirikiano
huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja
mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha
utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya
Chitego na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu
wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo
lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni waliokumbwa na
janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro ikiwa
ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulishughulikia tatizo
hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na ushirikiano
ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika
kushughulikia suala hili.
Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea
nchini hivi sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika
Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa
Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la
mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na
viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya
Madaktari. Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na
watarudi kwenye meza ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia
nilielezea matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi
yetu. Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa
tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa
sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma
tena.
Ndugu Wananchi;
Kama walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao
walirudi kwenye mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama
Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya
Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha Madaktari na
Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for
Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa
ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya
kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili
makubaliano yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku
ile ya tarehe 8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio
la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika
vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari.
Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:
- Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
- Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
- Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
- Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
- Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
- Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
- Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
- Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
- Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
- Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
- Huduma za afya ziboreshwe nchini.
- Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. La kwanza,
ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini. Serikali ilieleza kuwa
upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa
mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia
magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa
madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green
Card za Bima ya Afya. Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya
Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.
Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu
kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja
walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya
pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi. Uongozi wa juu wa Wizara
umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajanisha
hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa
kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na
Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza,
kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari
wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu
asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana
kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini.
Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali. Nililieleza hili
mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya
kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Endelea kusoma habari hii kwenye tovuti ya www.globalpublishers.info bofya hapo usome zaidi na zaidi.
No comments:
Post a Comment