Uhispania waliandikisha historia
kwa maarifa ambayo sio rahisi kuiga, kwa kuifunga Italia magoli 4-0
katika fainali ya Euro 2012 usiku wa Jumapili, mjini Kiev, Ukraine.
Licha ya mchezo mzuri wa Italia, vijana wa
meneja wa Uhispania, Vicente del Bosque walithibitisha kwamba kimataifa
wanaweza kujigamba wao ndio wenye mchezo bora zaidi duniani, kwa
kuzingatia namna walivyoichezea timu ya Italia, na kuwalazimisha
kusalimu amri.
David
Silva aliifungia Uhispania bao la kwanza, na kabla nusu ya kwanza ya
mchezo kumalizika, mchezaji mpya wa Barcelona, Jordi Alba aliandikisha
bao la pili, baada ya kukimbia kwa kasi na kumalizia kwa ustadi kabisa.
Ingawa Italia walikuwa na upungufu wa mchezaji
mmoja, baada ya kumpoteza mchezaji wa zamu wa tatu Thiago Motta baada ya
kujeruhiwa, walicheza kwa bidii, lakini wataalamu wa kandanda kwa
upande wa kupokezana mpira, Uhispania, waliwadunisha kabisa.
Fernando Torres aliingia kama mchezaji wa zamu,
na akafanikiwa kuubadilisha mchezo, na akiandikisha bao la tatu la
Uhispania, kabla ya mwenzake katika klabu ya Chelsea, Juan Mata,
kuandikisha bao la nne na la mwisho la Italia, na ambalo bila shaka
liliwavunja moyo kabisa mashabiki wote wa Italia.
Mchezo huo bila shaka umeyazima matamshi ya
baadhi ya watu ambao awali walimlazimu kocha wa Uhispania Del Bosque na
wachezaji wake kujitetea katika mkutano na waandishi wa habari, kabla
mechi ya fainali kuanza, kwamba mchezo wao katika mashindano ya Euro
2012 umekosa msisimko.
Lakini usiku wa Jumapili mambo yalikuwa tofauti.
Maarifa yote yaliyowawezesha kuwa mabingwa wa
Euro 2008 na vile vile Kombe la Dunia la mwaka 2010 nchini Afrika Kusini
yalijitokeza.
Ilikuwa ni fainali ambayo ilimvunja moyo kabisa
kocha wa Italia, Cesare Prandelli, lakini bila shaka haikuwa fedheha
kushindwa na timu yenye maarifa ya hali ya juu kiasi hicho.
Italia itaweza kujivunia namna ilifika katika
fainali, licha ya kushindwa kwa magoli mengi na timu ambayo ilikuwa ni
wazi imo katika kiwango cha pekee.
No comments:
Post a Comment