Afisa Muandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania Nd.
Juma Kimtu akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi Mchango wa Maafa wa Shilingi 10,000,000/- hapo ofisini kwake
Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Nyuma yake ni Meneja Msuluhishi wa
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khamis Phil Phil Than.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akipokea mchango wa Maafa wa shilingi 10,000,000/- kutoka kwa Meneja
Msuluhishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khamis
Phil Phil Than hapo katika Ofisi yake iliyopo Baraza la Wawakilishi
Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
---
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amewanasihi Wananchi kuendelea kuiamini Serikali katika kupokea
Taarifa zake hasa wakati wa kutokea Majanga na Maafa.
Nasaha hizo amezito hapo katika Ofisini yake iliyopo Baraza la
Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akipokewa mkono
wa Pole kutoka kwa Taasisi mbali mbali za Umma na Kijamii.
Salamu hizo za mkono wa pole zimetolewa kwa Balozi Seif na Uongozi
wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } na ule wa Hifadhi ya
Taifa ya Jamii ya Tanzania { NSSF } ambapo kila moja ilikabidhi mchango
wa Shilingi Milioni kumi { 1,000,000/- }.
Balozi Seif alisema Jamii kujenga tabia ya kuiamini Serikali
hupelekea kuwepuka kuchanganywa wakati wa kupokea Taarifa hizo kutoka
vyombo vya Habari vinavyopokea Baadhi ya Taarifa zisizo rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa mifuko
hiyo ya Hifadhi ya Jamii Bara na Zanzibar kwa kufikiria jambo hilo
muhimu la kutoa mchango ambalo Taifa linahitaji kuungwa mkono katika
kukabiliana nalo.
Aliuhakikishia Uongozi wa Taasisi hizo kwamba michango hiyo
itasimamiwa vyema kwa ajili ya kuwafika waliohusika kwa kutumia
utaratibu uliotumika wakati wa ajali iliyotokea Mwaka jana.
Alisema licha ya zoezi la uokozi kuwa na gharama kubwa lakini
Serikali inaendelea kutoa huduma zote za mazishi na usafirishaji wa
maiti zinazopelekwa Tanzania Bara ambazo zilipatikana kutokana na ajali
ya Meli ya M.V Skagit hapo juzi.
Aliongeza kuwa shughuli hiyo ikiwemo gharama za
vyombo, mafuta, Chakula na uokozi zinahitaji kuungwa mkono na taasisi na
jumuiya ya kiraia ndani na nje ya Nchi. “ Serikali imeshachukua jukumu
la kuzizika zile Maiti zilizoshindwa kutambulika hadi sasa,
kuzisafirisha maiti tatu hadi Tanzania Bara pamoja na familia nne wakati
maiti moja ya raia wa kigeni bado haijatambulika”. Alifafanua Balozi
Seif.
Alisisitiza kwamba katika juhudi za kukabiliana na tatizo
hilo wazamiaji wa Israel walioko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja
wameamua kusaidia kazi ya uokozi kwenya Meli hiyo ili kuendelea kutafuta
miili ya Watu iliyopotea.
Mapema Meneja Msuluhishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
Zanzibar { ZSSF } Ndugu Khamis Phil Phil Than alisema yapo mambo mengi
kwenye tukio hilo la Maafa ambayo yanahitajika kupata msukumo kutoka kwa
Washirika, Taasisi na Jumuiya za Kiraia. Ndugu Phil Phil alisema mfuko
wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar umekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza
majukumu yake yaliyolenga zaidi kwenye eneo la Jamii.
Naye kwa upande wake Ofisa Muandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii Tanzania { NSSF } kutoka Makao Makuu Mjini Dar es salaam Nd.
Juma Kimtu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi
hiyo imeamua kutoa mchango huo baada ya kuona uzito Maafa yaliyotokea
ambayo yameigusa Jamii yote.
Ndugu Kimtu alisema Serikali kwa kuwa ni
ya watu haina budi wakati wote kusaidiwa hasa katika masuala ya Majanga
na Maafa ambayo kwa kiasi kikubwa huigusa Jamii yote.
Na
Othman Hamisi Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili Wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment