VURUGU zimeibuka katika mtaa wa Mbondole, Kata ya Msongola,
Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, baada ya wavamizi kuingia katika eneo
lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule na kugawana maeneo kwa ajili
ya kujenga makazi ya kudumu.
Tukio hilo lilitokea jana baada ya kikundi cha watu wasiofahamika
kuvamia eneo hilo na kutenga makazi yao huku wakiligawa katika vipande
vya mita 20 kwa 20 kwa ajili ya wenzao ambao hawajawasili.
Mwenyekiti wa Tawi la Kulutini (CCM), Sefu Mbinga aliieleza Tanzania
Daima kuwa vurugu hizo zilisababisha wananchi wa eneo hilo na Chakenge
kushirikiana na kuungana kwa vita ili kulichukua eneo hilo kwa nguvu.
“Mbali na wavamizi hao kujipanga kuliteka eneo hilo, lakini bado
walidhamiria kuwadhuru wananchi, hivyo tulifanikiwa kujipanga vizuri kwa
kuchukua silaha kama mapanga, visu, sululu na nyingine, ili
kuwadhibiti,” alisema Mbinga.
Naye Katibu wa kamati ya uvamizi, Daniel Zacharia alisena waliamua
kuingia eneo hilo baada ya kubaini kuwa ni pori na halimilikiwi na mtu
au taasisi yoyote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime,
alibainisha kutopewa taarifa kuhusiana na sakata hilo, ila aliahidi
kulifuatilia na baadaye kulitafutia ufumbuzi wa kina.
No comments:
Post a Comment