WALIMU nchini leo wameanza mgomo kuishinikiza serikali
iwalipe madai yao mbalimbali ikiwemo ongezeko la mishahara kwa asilimia
100, posho ya kufundishia kwa walimu wa sayansi asilimia 55 na asilimia
50 kwa walimu wa masomo ya sanaa.
Wakati walimu wakianza mgomo wa leo, serikali imetangaza
kuwa mgomo huo ni batili kwa sababu shauri hilo liko katika Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ofisi ya Rais (Ikulu), kupitia kwa Kaimu
Katibu Mkuu Kiongozi, Peniel Lyimo, Julai 27 ilitoa taarifa kupinga
mgomo huo kwa madai kuwa ni batili, kwa sababu kuna kesi mahakamani
inayozihusu pande hizo mbili.
“Kwa sasa shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii
siku ya Ijumaa Julai 27, 2012 majira ya saa sita mchana pande zote mbili
zilifika mahakamani na mahakama ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe
maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne Julai 31, 2012 saa sita mchana ili
kuiwezesha mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa
uamuzi. Kwa hiyo mgomo huo si halali kwa vile shauri hilo bado liko
mahakamani,” ilisema.
Juzi Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba,
alitangaza kuwa leo wangeanza mgomo nchini nzima huku akiwasisitiza
walimu wasiogope kwa sababu taratibu zote za kisheria zimefuatwa.
Mukoba alisema Julai 28 (Ijumaa) mwaka huu, walimu walipiga kura ya
kugoma au kutokugoma ambapo walimu 183,000 walipiga kura na 153,848
sawa na asilimia 95 waliunga mkono kufanyika kwa mgomo.
Alisema walifikia hatua hiyo baada ya serikali na CWT kushindwa
kufikia makubaliano katika siku 30 walizoipa kuanzia Juni 25 mwaka huu.
Madai makubwa ya walimu katika mgomo huo, mbali na malimbikizo ya
madeni yao ya huko nyuma, pia wanataka ongezeko la mishahara kwa
asilimia 100, posho za kufundishia kwa walimu wa sayansi asilimia 55 na
walimu wa masomo ya sanaa asilimia 50 na posho za mazingira magumu
asilimia 30.
Maandalizi yaendelea
Hadi jana jioni viongozi wa mikoa mbalimbali walitangaza kuunga mkono
azimio la kugoma licha ya vitisho vilivyotolewa na serikali.
Katibu Mkuu wa CWT, mkoa wa Dar esSalaam, Abdallah Mkaula,
aliwataka walimu wa mkoa huo kubaki majumbani kwao mpaka watakapotangaziwa vinginevyo na viongozi wao.
Mkaula alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi za
kuwagawa walimu ili wasiwe na msimamo mmoja huku ikiendelea kukalia madai yao.
Mkoani Mara, Mwenyekiti wa CWT wa mkoa huo, Livingstone Gamba,
aliwataka walimu wote kuanzia leo kutoenda kazini, ikiwa ni pamoja na
kutokujaza fomu zitakazoletwa na mwajiri
Gamba alisema kuwa matumizi ya nguvu yanayofanywa na serikali si jibu,
bali utakomaza tatizo na walimu wasitishike na vitisho hivyo
No comments:
Post a Comment