KLABU ya Simba imemuuza kiungo
wake mshambuliaji, Mwinyi Kazimoto, katika timu ya Al-Markhiya Sports
Club ya Qatar kwa dau la dola 50,000 (zaidi ya shilingi milioni 81)
ambazo zaidi ya nusu zimeshakabidhiwa.
Kiungo huyo, hivi karibuni alitimkia huko kwa ajili ya kufanya majaribio kabla ya kusajiliwa na timu hiyo.
Akizungumza
na Championi Jumatano katika makabidhiano ya fedha hizo, Mwakilishi wa
Al-Markhiya Sports Club, Saleh Afif, alisema wametanguliza dola 35,000
(shilingi milioni 57).
Afif alisema fedha nyingine ambazo ni dola 15,000 (zaidi ya shilingi milioni 24) watazilipa mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.
Alisema staa huyo akiwa kwenye timu hiyo, anatarajiwa kulipwa mshahara wa dola 7,000 (zaidi ya shilingi milioni 11).
Mwakilishi
huyo alisema kiungo huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea
timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini huko.
“Kazimoto
amesaini kuichezea Al-Markhiya Sports Club ya Qatar kwa dau la dola
50,000 ambazo sehemu yake tayari leo (Jumatatu) tumezikabidhi kwa
mwenyekiti wao wa usajili, Hans Pope.
“Tumetanguliza fedha nyingine
ambapo dola 15,000 tutazilipa mwishoni mwa Desemba, mwaka huu. Akiwa
kwenye timu hiyo anatarajiwa kulipwa mshahara wa dola 7,000,” alisema
Afif.
Naye Hans Pope baada ya makabidhiano alisema kuwa wamemruhusu kiungo huyo kwenda kuichezea timu hiyo.
Hans
Pope alisema hawawezi kumzuia kiungo huyo kwenda kucheza soka nje ya
nchi, pia ameitaka timu hiyo kutorudia kitendo walichokifanya cha
kumtorosha kambini Kazimoto na kumpeleka huko Qatar kwenye majaribio.
“Sisi
hatuwezi kumzuia mchezaji yeyote kwenda kucheza soka nje ya nchi,
kikubwa kinachotakiwa ni timu kufuata taratibu na siyo mlivyofanya kwa
Kazimoto, kumtorosha kwenye kambi ya Stars na kumpeleka huko Qatar
kwenye majaribio,” alisema Hans Pope.
No comments:
Post a Comment