CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimelishutumu Bunge na Serikali
kwa kuiingilia uhuru wa Mahakama kwa matamko yao kuwa mgomo wa walimu
unaoendelea hivi sasa nchini ni batili.
Chama hicho pia kimelaani ufujaji wa fedha za umma unaofanywa na
watendaji wa serikali kwa kutoa matangazo katika vyombo vya habari
yanayoelezea kuwa mgomo huo si halali.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba, ndiye aliyetoa kauli hiyo jana jijini Dar
es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea
mgomo, vitisho na kukamatwa kwa baadhi ya walimu wanaoutekeleza.
Mukoba alisema mgomo wao ulizingatia kifungu cha 80(1) cha sheria ya
ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, hali iliyoifanya serikali
kukimbilia mahakamani kwa lengo la kuomba mahakama kutoa zuio kwa CWT
kutoendelea na mgomo huo.
Alisema wakati suala hilo likiwa mahakamani na kabla halijaamriwa
serikali kupitia kwa watendaji wake, akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky
Sadiq, wakaingilia uhuru wa mhimili mwingine kwa kuutangazia umma kuwa
mgomo ni batili.
“Tumesikitishwa kuona Bunge lenye dhamana ya kuisimamia serikali nalo
limeamua kuingilia uhuru wa mahakama kwa lengo la kuisaidia serikali
pale Naibu Spika, Job Ndugai, alipoitangazia jamii kuwa mahakama
ingetoa hukumu Julai 31, saa saba mchana wakati pande zote mbili
zilikuwa hazijasikilizwa,” alisema.
Vitisho, kukamatwa
Akizungumzia vitisho na kukamatwa kwa walimu walio katika mgomo,
Mukoba alisema tayari wamepokea taarifa za sehemu mbalimbali kuwa walimu
wanakamatwa na kulazimishwa kufundisha, hili si jambo jema.
Alitaja baadhi ya mikoa inayofanya vitendo hivyo kwa walimu ni Pwani,
Morogoro na Ruvuma ambapo viongozi na watendaji wa CWT wanapewa vitisho
na wakuu wa mikoa pamoja na kamati za ulinzi za mikoa.
Alisema katika wilaya za Tarime, Rungwe, Kyela na Babati viongozi wa
CWT wameshakamatwa huku mkoani Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Sadik
amewatisha wanachama na viongozi huku akiamrisha wakamatwe.
Mukoba alisema Sadiq ameudanganya umma kuwa yeye (Mukoba) aliripoti
katika kituo chake cha kazi ambacho ni Shule ya Benjamin Mkapa na
kusaini daftari la mahudhurio lakini baadaye alianza kuwazuia wenzake
wasiende kazini.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo ya mkuu huyo wa mkoa imelenga kumchafulia
jina ili aonekane msaliti mbele ya jamii na hasa walimu ambao sasa
wanaendelea na mgomo kudai haki zao.
Hali ya mgomo
Mukoba alisema hadi sasa walimu wamegoma kwa asilimia 95 na
wameshindwa kufikia asilimia 100 kwa kuwa kila sehemu kuna wasaliti
ambao wakati mwingine hawana nia hiyo bali wamezaliwa waoga wa kupigania
masilahi yao.
“Tunajua wapo wanaoshindwa kusimamia haki yao kwa dhana ya
kujipendekeza ili wafikiriwe katika madaraka mengine, wengine hawaoni
mbele na pia wapo wasaliti na hawa hawakosekani kwani walikuwapo hata
enzi ya mitume,” aliongeza Mukoba.
Mukoba alitoa wito kwa serikali kuwaachia huru walimu wote
waliokamatwa na badala yake itafute njia sahihi ya kutatua tatizo kwa
kuwa suala hilo lipo mikononi mwao.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona serikali ikifunga milango kwa
ajili ya kukutana na walimu na badala yake ikidhani njia ya mabavu ndiyo
suluhisho la kumaliza mgogoro huo.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment