Serikali imesema haina nia ya kuwafukuza madaktari 374 waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo katika hospitali mbalimbali nchini baada ya mgomo wao.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando, alisema serikali haina nia hiyo.
Alisema hadi sasa hakuna daktari aliyefukuzwa kazi kutokana na mgomo huo na hakuna pia aliyefutiwa usajili wake wa kudumu.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu huyo, serikali ilichokifanya kwa madaktari hao ni kuwahoji, na kazi inayoendelea sasa ni kuyafanyia kazi majibu yao na kisha kuwaita mmoja mmoja kwenye Baraza la Madaktari Tanganyika ili wakajitetee dhidi ya mashitaka yatakayo wakabili na hatua za kisheria zitafuata lakini si za kufukuzwa.
"Zipo adhabu mbalimbali zinatakiwa kufuatwa na sio kuwafukuza kazi na serikali haina malengo hayo ya kuwafukuza. Kumekuwa na uzushi usio na maana kuwa madaktari wamefukuzwa kazi, sisi tunatambua umuhimu wao," alisema Dk. Mmbando.
Dk. Mmbando alisema kitendo cha madaktari hao kuambiwa kuwasilisha usajili wao wa muda, sio kwamba wamefukuzwa kazi, bali ni utaratibu katika masuala ya kazi.
Alisema hata daktari anapohamishwa na kupelekwa eneo jingine, ni lazima awasilishe usajili huo wa muda ambao ulikuwa umempa maelekezo ya kuwa katika hospitali husika.
"...hivyo kitendo cha kuwaambia walete usajili wao sio tumewafukuza, na ujue ule ni usajili wa muda na sio ule wa kudumu," alisisitiza.
Alisema mchakato wa zoezi hilo unaendelea vizuri na hivi karibuni wataitwa kwenye Baraza la Madaktari Tanganyika ili wajitetee.
Mmoja wa madaktari hao ambaye alizungumza na NIPASHE Jumapili, ambaye kwa sasa yuko mitaani, alisema hawajui hatma yao licha ya serikali kuwanyang'anya usajili wao wa muda.
Daktari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema bado hawajajulishwa ni lini wataitwa kwenye baraza hilo ikizingatiwa kuwa muda unaendelea kusogea na kwamba wanahofia kuupoteza ujuzi wao kwa kuwa walikuwa mafunzoni.
Awali madaktari hao walitakiwa kurudisha usajili wao wa muda kutokana na mgomo wao.Madaktari hao walipewa usajili wa muda ili kuwawezesha kufanya mafunzo yao kwa vitendo (internship) katika hospitali mbalimbali nchini, lakini wanadaiwa kufanya mgomo Julai 23 hadi 29, mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu aliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la Madaktari Tanganyika ambapo msajili wa baraza hilo aliwaandikia kila daktari aliyelalamikiwa barua ya kuwasilisha usajili wao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment