Chadema yakutana leo kwa dharura.
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, inakutana leo kwenye kikao cha dharura kujadili hali ya siasa nchini na kufanya maamuzi ya hatua zaidi za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Chadema, Kurugenzi ya Habari na Uenezi, Tumaini Makene ilisema kikao hicho kinafuatia mfululizo wa matukio ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwenye shughuli halali (kwa mujibu wa katiba ya nchi) za chama na njama za CCM na baadhi ya viongozi wa Serikali kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa mbinu haramu.
Ilieleza kuwa hivi karibuni baada ya mauaji ya Ali Singano (Zona) mjini Morogoro, yaliyosababishwa na Jeshi la Polisi mkoani humo wakati walipoingilia kwa nia ya kuvuruga mapokezi na mkutano wa Chadema, chama kilitoa kauli kumtaka Rais Jakaya Kikwete aagize kutumika kwa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo ili kubaini chanzo na kuondoa utata wa kifo cha kijana huyo.
Aidha, baada ya mauaji ya mwandishi wa habari wa Channel Ten na Magic FM, Daudi Mwangosi, Chadema kilitoa tamko kumtaka Rais Kikwete, aagize kufanyika uchunguzi huru kupitia tume ya kimahakama. Kwani katika tukio hilo hakukuwa na utata kuwa mwandishi huyo aliuawa na polisi. Hivyo uchunguzi huru ulihitajika ili kubaini vitu vya ziada, kama vile kwa nini kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa katiba, haki za binadamu na sheria za nchi na nani alitoa amri za mauaji hayo.
“Chadema kilipinga kuundwa kwa kamati ya kuchunguza tukio la kuuawa kwa Mwangosi, iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, kwa sababu iliundwa kinyume cha sheria ya tume za uchunguzi, ikiwa na lengo la kufunika mambo na kurejesha uhusiano wa serikali na vyombo vya habari, badala ya kutafuta ukweli. Kwa mara nyingine tena kilimtaka Rais Kikwete aunde tume huru ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria ili kweli tupu ijulikane,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema wakati chama kikitangaza kuahirisha kwa muda mikutano ya
Operesheni Sangara-Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), mjini Iringa, kilisisitiza kauli yake ya kumtaka Rais Kikwete kuingilia kati kuhakikisha analinda katiba ya nchi inayotambua haki ya kuishi, kwa kuagiza uchunguzi huru ufanyike ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuzuia hali hii ya vyombo vya dola kufanya mauaji ikiwa na lengo la kutisha wapinzani na wakosoaji wa serikali ya CCM.
Imefafanua kuwa kutokana na ukimya wa Rais Kikwete katika matukio hayo na mengine ya namna hiyo ambapo raia wasiokuwa na hatia wametekwa, kuteswa na kuuawa na vyombo vya dola au wakiwa mikononi mwa vyombo hivyo, Chadema katika kikao chao cha leo kufanya maamuzi ya hatua zaidi za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi na Serikali inayoongozwa na CCM, kwa manufaa ya taifa Watanzania wote kwa ujumla.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment