WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi, anatarajia kuzindua mashine ya kisasa ijulikanayo kama MRI, inayotumika kupiga picha za sehemu za ndani ya mwili wa binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dkt. Parul Chhaya, alisema wamefikia uamuzi huo wa kununua mashine hiyo ili waanze kutoa huduma hiyo ambayo imekuwa tatizo kubwa hapa nchini. Alisema kutokana na kutokuwapo kwa mashine hiyo, wagonjwa walikuwa wakisafiri kwenda nje ya nchi ili kupata matibabu yaliyokuwa yakitokana na mashine hiyo.
“TMJ tumeona kuna sababu ya kuongeza vifaa muhimu katika huduma zetu za kila siku na kadri siku zinavyozidi kwenda, tunakutana na changamoto mbalimbali, hasa ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya haraka, ili kuokoa maisha yao. Katika suala la matibabu kuna kila sababu ya kujipanga na kuwa na malengo ya kuongeza vifaa muhimu, kama mashine hiyo ambayo ipo tayari kuanza kazi ya kuwasaidia Watanzania wanaopata matatizo yanayohitaji huduma ya kifaa hicho,” alisema Chhaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Arrwa Jaffji, alisema TMJ imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wagonjwa na wateja wake, hali ambayo imefanya hospitali hiyo kuaminiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
“Tunatambua umuhimu wa afya ya mwili ambayo ndio huduma inayotolewa na TMJ na kwa sababu hiyo, tumekuwa tukipambana kwa kila hali kuhakikisha tunafanikiwa kupata kifaa hiki ambacho Watanzania wengi wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya kifaa hiki,” alisema Jaffji.
Aliongeza kuwa, huduma ya CT SCAN itakuwa inatolewa katika hospitali hiyo baada ya uzinduzi wa kifaa hicho na kwamba TMJ, itakuwa ni kituo cha pili cha afya kuwa na kifaa hicho, ikiwa imetanguliwa na Hospitali ya Aga Khan pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
via MTANZANIA
No comments:
Post a Comment