Na Raymond Kaminyoge Zaina Malongo, gazeti la Mwananchi - Dar es Salaam -- WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia na kutumia mbinu za uhalifu wa hali ya juu na kupora magunia ya fedha kutoka Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), iliyopo barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo linaloweza kufananishwa na filamu za kimafia, lilitokea jana kati ya saa 2.30 na saa 2.45 asubuhi. Waliondoka na magunia hayo wakiwa wameyapakia kwenye magari yao ya kifahari, bila kuua wala kujeruhi mtu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alithibitisha tukio hilo na kusema fedha walizoiba zinakadiriwa kuwa zaidi ya Shilingi Milioni 400, “Hatufahamu kiasi kamili lakini, tulivyowahoji maofisa wa benki wanasema ni zaidi ya Sh400 milioni ambazo zimeibiwa,” alisema Kova na kwamba tayari meneja wa benki, msaidizi wake na mlinzi aliyekuwa zamu wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema watuhumiwa hao wa ujambazi, waliingia kwenye benki hiyo, huku wakiwa wamevalia vitambusho vya benki kujifafanisha na wafanyakazi wa benki hiyo, mbinu ambayo iliwahadaa watu waliokuwa kwenye eneo hilo wasishtuke kwa lolote. Vitambulisho hivyo viliwafanya walinzi wa benki hiyo kutokuwa na wasiwasi na watuhumiwa hao, jambo lilitoa fursa kwao kutekeleza uhalifu katika mazingira ya urahisi zaidi. Baada ya kuingia ndani ya benki, majambazi hao wakiwa na bastola yaliwaweka chini ya ulinzi walinzi wa benki hiyo.
Wakati hayo yakitokea mmoja wa majambazi hao aliamuru wafanyakazi wa benki hiyo kuendelea kuwakaribisha wateja wao na kila aliyekuwa akiingia aliwekwa chini ya ulinzi. Mtuhumiwa mwingine wa ujambazi akiwa na bastola, alimfuata mtunza funguo wa chumba maalum cha kuhifadhia fedha na chumba cha Mashine za Kutolea Fedha (ATM) na kumwambia, atoe funguo, “Tena jambazi huyo alimtaja kwa jina mtunza funguo huku akisema naomba funguo za strong room tumekuja kuchukua fedha zetu,” alisema mmoja wa mashuhuda akimkariri jambazi huyo na kusema alipewa funguo bila kizuizi.
Baadaye majambazi hao walifanikiwa kufungua kwenye vyumba hivyo na kuchukua fedha zote na, kuzihifadhi kwenye magunia manne. Wakati shughuli hiyo ikiendelea majambazi wengine waliharibu mitambo ya kamera zinazoonyesha watu wanaoingia na kutoka kwenye benki hiyo, “Tunajua mnaturekodi kwenye kamera zenu na sisi tunaifahamu vizuri teknolojia hii, ndiyo maana tunalazimika kuharibu mtandao mzima,” mmoja wa jambazi alikaririwa akisema huku akifungua mtambo wa kamera.
Baada ya kumaliza kuharibu mitambo ya kamera, waliondoka na maguni ya fedha na kwenda walikoegesha magari yao ya kifahari na kupakia.
Walioshuhudia walisema, majambazi hao walikuwa wakitumia magari matatu ya aina ya Toyota Land Cruiser, Nissan Patrol na Toyota Noah na kwamba, wakati wakitekeleza ujambazi huo madereva wote walikuwa wamebaki kwenye magari hayo yaliyokuwa yameegeshwa karibu na benki hiyo. Baada ya magari hayo kupakia magunia hayo, madereva hao waliyaondoa magari hayo kwa kasi kuelekea eneo la katikati ya jiji. Wameendelea kusema kwamba wakati majambazi hayo yanaondoka katika eneo hilo mnamo saa 2.45 asubuhi, hakukuwa na msongamano wa magari katika barabara ya Nyerere kama kawaida, “Unafahamu muda huu eneo hili huwa na msongamano wa magari lakini, tunashangaa wakati tukio hili linatokea hakukuwa na magari hadi tukadhani labda kuna msafara wa viongozi,” alisema mmoja wa mashuhuda.
Baada ya tukio hilo kumalizika maofisa wa Jeshi la Polisi walifika katika benki hiyo iliyopo kwenye jengo la Jamana wakiongozwa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova.
No comments:
Post a Comment