Baada ya Msajili wa vyama vya siasa Bwana John Tendwa juzi kusema kuwa vyama vya siasa vitakavyobainika kusababisha mauaji vitafutiwa usajili kutokana na kukiuka sheria, kanuni na utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za siasa nchini, MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, amemjia juu Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini, John Tendwa na kusema kauli yake aliyoitoa dhidi ya vyama vya siasa ni ya kukurupuka.
Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na gazeti la MTANZANIA jana kwa simu na kusema kuwa, kauli ya Tendwa ya kutishia kufuta vyama vya siasa imejaa vitisho.
“Tendwa ni mkurupukaji wa siku nyingi sana, anawezaje kusema atakifuta chama cha siasa wakati yeye hana chombo cha kufanya uchunguzi, suala la kifo ni suala la jinai yeye anasemaje anafuta chama? Ukiangalia vifo vingi au hiki kifo cha Mwandishi Daudi Mwangosi ni wazi polisi wamehusika kwa sababu bomu limehusika na lile bomu lilitoka kwa polisi na picha zimeonyesha kwamba polisi ndiyo wamehusika. Sasa kwa mazingira haya, yeye anawezaje kusema anakifuta chama kilichokuwa na shughuli zake katika eneo hilo?,” alihoji Profesa Lipumba.
Alisema kauli ya Tendwa ina lengo la kuhujumu shughuli za kisiasa hapa nchini na kwamba inapaswa kupingwa na vyama vyote vyenye lengo la kuimarisha demokrasia.
“Hii kauli yake ni ya kifisadi kwa sababu anataka watu wamuabudu, unapoona mtu anataka kuabudiwa basi ujue kabisa ana sifa zote za kifisadi kwa hiyo huyu ni fisadi hana tofauti na mafisadi wengine ambao wanadhuluma rasilimali za nchi. Huyu amekuwa mkurupukaji wa siku nyingi sana, hakuna asiyemjua na kauli yake hii ni kutaka kufinya demokrasia, yeye aache vyombo vya dola vifanye uchunguzi wake, ili kufahamu ni nani amehusika katika matukio hayo ambayo yamesababisha vifo vya raia. Yeye afanye kazi yake ya kusajili vyama na si kuingilia masuala ya jinai, ambayo yana mamlaka husika na kufahamu kifo kimesababishwa na nani wala si kusema unafuta vyama vya siasa, hii ni kauli isiyokuwa na mashiko kabisa,” alisema Profesa Lipumba.
Juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Tendwa alisema atavifuta vyama vya siasa vinavyosababisha mauaji wakati wa shughuli zake za kisiasa.
Pamoja na mambo mengine, Tendwa alikuwa akizungumzia kifo cha Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi aliyefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa bomu na askari polisi katika kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa mwanzoni mwa wiki hii.
via Mtanzania
No comments:
Post a Comment