ENEO la Hospitali ya Mwananyamala katika Manispaa ya Kinondoni, jana liligeuka la vurugu kwa muda, baada ya ndugu kuchachamaa wakitaka kukabidhiwa mwili wa mpendwa wao baada ya kuelezwa kuwa, umeshachukuliwa tayari kwa maziko mkoani Tanga.
Wanandugu hao wa jijini Dar es Salaam, waliwasili hospitalini hapo jana asubuhi kwa lengo la kukamilisha taratibu za kumzika ndugu yao kwenye makaburi ya Mikocheni, Manispaa ya Kinondoni.
Tukio hilo lililosababisha mtafaruku mkubwa kati ya wanandugu na madaktari katika hospitali hiyo na hata kuwalazimu polisi wa kituo cha Mwananyamala kuingilia kati, limethibitishwa na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela na kuongeza kuwa, limechangiwa na uzembe wa mhudumu katika chumba cha kuhifadhia maiti.Aliongeza kuwa, juhudi za kuufuatilia mwili huo zinaendelea na kwamba, kama utakuwa umezikwa, kitaombwa kibali maalumu cha mahakama ili ufukuliwe na kisha ukabidhiwe kwa ndugu.
Awali, Fredrick Nkenzidyo ambaye ni kaka wa marehemu, alisema ilikuwa wauchukue na kuuzika mwili wa marehemu katika makaburi ya Mikocheni jana, lakini cha kushangazwa waliambiwa kuwa mwili huo haupo.lisema kuwa akiwa hospitalini hapo, alipewa taarifa kuwa kuna watu waliwasili asubuhi na kujitambulisha kuwa ni ndugu wa marehemu na kuondoka na mwili huo.Akizungumzia kuhusiana na marehemu alisema ndugu yao alikuwa akiitwa Ntimaruku Nkenzidyo na alikuwa mlinzi wa kampuni ya Group 7 Security na alikutwa na mauti kufuatia ajali ya gari iliyotokea Masaki, Dar es Salaam Septemba 17, mwaka huu.
Alisema kuwa baada ya ajali hiyo, mwili wake ulipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kuhifadhiwa na hata walipokuwa wakifika kuangalia mwili walikuwa wakiukuta katika sare zake za kazi za kiuaskari.Akizungumza kwa jazba mbele ya polisi waliofika hospitalini hapo, alisema wameelezwa mwili wa ndugu yao umepelekwa Tanga na watu walisingizia kuwa ni ndugu yao na hatimaye kukabidhiwa mwili wa marehemu.Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa hakukuwa na ujanja wa kuusafirisha mwili huo, bali kulikuwa na makosa yaliyoanzia kwa wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt. Sophinias Ngonyani hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, huku akionekana kuzunguka huku na huko kutafuta chanzo cha tukio hilo.Kufikia mchana, huku ndugu wakipaza sauti za kuutaka mwili wa ndugu yao kiasi cha kuwapa kazi ya ziada askari polisi, busara ilitumika kwa pande tatu, yaani uongozi wa hospitali, ndugu wa marehemu na polisi kuingia katika chumba maalumu kwa ajili ya majadiliano ambayo yalifikia mwafaka wa kusubiri juhudi za kuurudisha mwili kutoka Tanga.
via HabariLeo
No comments:
Post a Comment