Na Raymond Kaminyoge, MWANANCHI -- WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, inawasaka wanaochapisha ramani za Tanzania kinyume na taratibu ili wachukuliwe hatua za kisheria.Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara hiyo, Dkt. Selassie Mayunga alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba ni wizara hiyo tu ndiyo yenye mamlaka kisheria ya kuchapisha ramani za Tanzania na kuzisambaza.
Dkt. Mayunga alisema kumekuwapo na kampuni na taasisi mbalimbali zinazochapisha ramani hizo na kuzisambaza kinyume na sheria, “Tunatangaza rasmi kwamba ramani hizo ni feki hazitakiwi kutumiwa na watakaobainika sheria itafuata mkondo wake.”Alisema watashirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwakamata wahusika na kuziondoa kwenye mzunguko ramani hizo.Mayunga alisema jambo la kusikitisha ni kwamba, hata taasisi za umma na za binafsi zinatumia ramani hizo feki bila kufahamu kwamba ni kinyume na sheria, “Ramani halali ni ile iliyotolewa na kuchapishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tu na si vinginevyo,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema wizara hiyo imetoa ramani mpya itakayojumuisha mikoa na wilaya mpya zilizotangazwa na Serikali. Mwaka jana Serikali ilitangaza mikoa mipya minne ambayo ni Njombe, Geita, Simiyu, Katavi na wilaya 19 ambazo kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo zitakuwa katika ramani mpya ambayo inaonyesha mipaka yake. Alisema taasisi za Serikali na watu binafsi wanatakiwa kuwasiliana na wizara hiyo kwa ajili ya upatikanaji wa ramani hizo.Akizungumzia mpaka wa Tanzania na Malawi katika ramani hiyo mpya, Dkt. Mayunga alisema mpaka uko katikati ya Ziwa Nyasa, “Mpaka wa Tanzania na Malawi uko katikati ya Ziwa Nyasa kama ulivyoonyeshwa katika ramani za zamani,” alisema.
No comments:
Post a Comment