MKAZI wa kijiji cha Isulilo katika wilaya ya Maswa, ameuawa na kisha mwili wake kuchomwa moto baada ya kumbaka mtoto wa miaka sita.Taarifa zilizopatikana kijijini hapo na kuthibitishwa na ofisa mtendaji wa kata ya Isanga, Charles Nghubuyabano, zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3:00 asubuhi.
Kijana aliyeuawa alitajwa kuwa ni Ndaki Ndaki (25) ambaye alikuwa akifanya kazi ya kuchunga mifugo kijijini hapo akitokea katika wilaya ya Bariadi.Nghubuyabano alisema kuwa siku ya tukio, Ndaki akiwa katika kazi yake hiyo, alimwona mtoto huyo na kisha kumkamata na kuanza kumbaka katika moja ya vichaka vilivyokuwa karibu na eneo hilo.“Wakati akiendelea na unyama wake huo, mtoto huyo alikuwa akilia kutokana na maumivu aliyoyapata kwani kitendo hicho kilimsababishia kutoka damu nyingi sehemu za siri na hivyo kuamua kumnyonga na kumuua ili kupoteza ushahidi,” alisema.
Baada ya kumaliza unyama wake huo baadhi ya watu waliosikia sauti ya mtoto, walianza kufuatilia kujua ni kitu gani kilichomsibu ndipo walipomkuta Ndaki akijaribu kuuhifadhi kichakani mwili huo.
Baada ya kugundua kuwa amejulikana aliamua kukimbia lakini alikamatwa na alipohojiwa alikiri kubaka na kisha kuua na hivyo wananchi hao walianza kumshambulia kwa kumpiga kwa kutumia mawe na silaha za jadi hadi alipopoteza maisha na kisha kuuchoma mwili wake kwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Salum Msangi, alikiri kutokea kwa tuki hilo na kuwaomba wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi.
Habari na na Samwel Mwanga, Maswa
Habari na na Samwel Mwanga, Maswa
No comments:
Post a Comment