Zaidi ya abiria 10 akiwemo askari polisi mmoja wanahofiwa kufariki dunia huku wengine tisa wakijeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Adventure lenye namba za usajiri T 294 ABD aina ya Scania walilokuwa wakisafiria kuteketea kwa moto katika kijiji cha Nyantakala wilayan Biharamulo mkoani Kagera.Ajali hiyo imetokea jana saa 4:30 asubuhi wakati basi hilo likitokea mkoani Mwanza kwenda Kigoma. Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo ambao wamelazwa kwenye hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo wamejeruhiwa vibaya akiwemo wakala wa kukatisha tiketi wa basi hilo, Dotto Tryphone (30), ambaye amevunjika miguu wakati wakijinasua kutoka kwenye basi hilo.
Kwa mujibu wa wakala huyo, basi hilo lilikuwa na abiria 54 waliokuwa wamekaa kwenye viti na abiria ambao hawakuweza kutambulika idadi yao waliokuwa wamesimama kutoka mwisho wa gari hadi mlangoni kutokana na basi hilo kujaza abiria zaidi ya uwezo wake.Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera, Paulo Alex Kalangi, alisema atatoa taarifa baadaye kwa kuwa alikuwa safarini kwa ajili ya ufuatiliaji wa ajali hiyo. Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wakiwemo majeruhi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya basi hilo kufika kwenye tuta la kuzuia mwendo kasi ambapo ghafra walianza kuona moshi ukitokea ndani ya basi kabla ya kushika moto na kuanza kuteketea. Dereva wa basi hilo ambaye hakutambulika jina lake haijajulikana kama alikimbia au aliteketea kwenye basi hilo mara baada ya kutokea ajali hiyo.
Mganga Mkuu msaidizi wa hospitali hiyo, Dk. Gabriel Mashauri, alisema amepokea majeruhi tisa na kwamba saba kati yao walikuwa katika hali mbaya, lakini bado wanaendelea kupatiwa matibabu. Aliwataja majeruhi waliolazwa kuwa ni Phinihas Elias (37), Pius John(21), Msigwa Isaya (18), Johary Chapa (23),Josephina Ngereza (46), Rashidi Mahonda (48) na Eles Ngereza(60).Waliovunjika miguu wametambulika kwa majina ya Dotto Tryphone (30) mkazi wa Nyakanazi na Zainabu Issa, wote wamevunjika miguu ya kushoto.
No comments:
Post a Comment