Moses Ng’wat, akiagana na mzee Nyimbo mara baada ya mkutano na waandishi wa habari wa mbeya na Iringa
TUKIO la kuuawa kwa mwandishi wa habari wa
kituo cha televisheni cha Channel ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi,
limeendelea kuibua mambo mapya, baada ya aliyekuwa mgombea wa ubunge wa
jimbo la Njombe Magharibi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kudai chama chake kilishiriki mauaji hayo kwa asilimia 50 na
asilimia nyingine 50 ilifanikishwa na Serikali kupitia Jeshi la Polisi.
Nyimbo alitoa kauli hiyo jana wakati
akizungumza na wandishi wa Habari Jijini Mbeya katika mkutano wake
aliouandaa kwa nia ya kutangaza nia yake ya kujiuzulu uanachama wa
Chadema na kubakia mwanasiasa huru asiye na chama.
Alisema kuwa Chadema hawakuwa na sababu ya
kwenda kuzindua tawi la chama hicho katika kijiji cha Nyololo wilayani
Mufindi kwa sababu tawi hilo alikuwa tayari alishalizindua yeye mwenyewe
miezi mitatu kabla ya kutokea kwa mauaji ya marehemu Mwangosi.
“Asilimia hamsini, mauaji ya rafiki yangu
Marehemu Mwangosi yalisababishwa na Chadema kwa kutotii amri ya Jeshi la
Polisi na kupanga kwenda kuzindua tawi la chama ambalo mimi nikuwa
tayari nimekwishalizindua miezi mitatu iliyopita kabla ya tukio lile,”
alisema Nyimbo.
Nyimbo alisema kuwa tabia ya viongozi wa
kitaifa wa Chadema kutoka makao makuu ya Chama Jijini Dar es Salaam na
kwenda mikoani kufanya mikutano ambayo huwa haijafanyiwa maandalizi
yoyote na wenyeji wao, hali ambayo inawafanya walazimike kufanya
maandalizi wao wenyewe, ndiyo inayosababisha migongano isiyokuwa ya
lazima na Jeshi la Polisi na hatimaye kuwa chanzo cha vurugu kwenye
mikutano ya chama hicho.
Alisema kuwa kwa kawaida mikutano ya siasa
inapaswa kuandaliwa na wenyeji kwa kuwa ndio ambao wanaofahamiana vizuri
na uongozi wa Jeshi la Polisi katika eneo husika kwa kuwa wao wakikaa
na kuzungumza huelewana, lakini suala hilo linapoingiliwa na wageni
husababisha viongozi wa sehemu husika kuwa na wasiwasi wa usalama na
hivyo kutokea migongano inayosababisha kutokea kwa vurugu.
Akizungumzia ushiriki wa Jeshi la Polisi
katika mauaji ya Mwangosi, Nyimbo alisema kuwa haikuwa sahihi kwa
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (RPC), Michael Kamuhanda kuingilia
kati suala hilo kwa kuwa sheria ya mikusanyiko inaeleza wazi kuwa mwenye
jukumu hilo ni Mkuu wa Polisi wa eneo linalofanyika tukio ambaye
alipaswa kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).
Alisema kuwa ikitokea OCD akazidiwa nguvu
au kushindwa kutoa maamuzi kwa suala husika ndipo hulazimika kuomba
msaada kwa bosi wake ambaye ni RPC ambaye naye anastahili kutoa
maelekezo na sio kwenda moja kwa moja kwenye eneo la tukio kama
alivyofanya Kamuhanda.
Kwa mujibu wa Nyimbo, hata tume iliyoundwa
na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kuchunguza
chanzo cha mauaji hayo ilikuwa ni batiri kwa sababu Dk. Nchimbi ni
sehemu ya watuhumiwa kwa upande wa Serikali.
Alisema kilichotakiwa kufanyika baada ya
kutokea kwa tukio hilo ilikuwa ni uwakamata viongozi wote wa Chadema na
viongozi wa Polisi waliokuwa eneo la tukio na kuwaweka ndani kwa muda
kupisha uchunguzi wa tukio hilo na pia kuwapa fundisho wasijaribu
kuchezea roho za watanzania na amani ya taifa.
Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa
Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC) aliuawa kwa kulipuliwa
na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu wakati akiwa kazini katika kijiji cha
Nyororo wilayani Mufindi ambako Chadema walikuwa wakizindua tawi la
chama hicho kijiji hapo.
Na Moses Ng’wat,Mbeya. picha na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment