Mtoto wa miaka 11 aliyekuwa anasoma Darasa la Sita katika Shule ya Msingi ya Mbezi wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, amedaiwa kubakwa na babu zake wawili wenye umri wa zaidi ya miaka 50.
Kutokana na hali hiyo, mama wa mtoto huyo (wote majina tunayo), anatishiwa maisha na ndugu wa mwanamume aliyezaa naye baada ya kutoa siri za kubakwa kwa mtoto huyo.
Mama huyo amedai kutaka kugeuziwa kesi baada ya kushitaki polisi vitendo vya ubakaji alivyofanyiwa mwanawe na babu zake wawili wa upande wa baba anaodai wana umri zaidi ya miaka 50 kwa nyakati tofauti, Julai na mapema mwezi huu (Oktoba).
Akizungumza jana, mama mzazi wa mtoto anayedaiwa kufanyiwa vitendo hivyo na babu zake wawili, mkazi wa Mbezi, Malamba Mawili, Dar es Salaam, alidai mwanawe alibakwa na alipoamua kuchukua hatua polisi, sasa anatishiwa na ndugu wa mwanamume.
“Mwanamume niliyezaa naye mtoto huyo (jina tunalo) tuliachana, mwezi mmoja uliopita akaja kumfanyia uhamisho mtoto kwenda Gongo la Mboto anakoishi kwa vile mtoto ana zaidi ya miaka saba, sikukataa niliposikia japo hakunishirikisha, lakini tangu amemhamisha mpaka leo shule hajaanza,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Wiki mbili zilizopita, nilipigiwa simu na baba wa mtoto wangu kuwa mtoto ametoroka, nikaenda na tukatoa taarifa Kituo cha Polisi Gongo la Mboto, niliporudi nyumbani kesho yake, wakanipigia amepatikana kwa babu yake mdogo katika familia ya babu mzaa baba yake, wakiniomba niende tukaongee maana kuna jambo limetokea.”
Mama huyo alisema alipokwenda, alikuta kuna kikao cha ndugu wa mwanamume na walianza kumwomba radhi wakimueleza kuwa mtoto alitoroka baada ya kuingiliwa kimwili na babu ndugu wa familia (jina tunalo) na walimtaka wamalize suala hilo kifamilia.
“Mtoto alipohojiwa alikiri kweli kubakwa na babu huyo na walisisitiza nisamehe huku wakimtaja Mungu, lakini mimi nikasema hilo ni kosa la jinai, tulipotoka nikaenda Polisi Mbezi kwa Yusuf ili mtoto ahojiwe na kisha hospitali ya Serikali ya Mbezi kumpima mwanangu,” alidai mama huyo.
Alisema vipimo vya hospitali vilihakikisha kweli mtoto alibakwa, lakini akawa hana ujauzito wala UKIMWI na mtoto alipohojiwa polisi, alikiri kubakwa na kueleza kuwa vitendo hivyo alikuwa akifanyiwa pia na babu mdogo wa mwisho kwa babu yake Julai mwaka huu.
“Kinachonisikitisha ni kwamba, yule mgambo aliyenisaidia kuwapata watuhumiwa hadi kuwafikisha polisi, sasa amekamatwa na watuhumiwa wapo huru, kama haitoshi, ndugu wa mwanamume wananitumia ujumbe wa simu wa kunitishia kuwa watahakikisha wananigeuzia kesi, naomba Serikali inisaidie katika hili,” alilalamika mama huyo.
Alisema pia Polisi wamekuwa wakimpiga danadana kuhusu suala hilo akiwafuata kuulizia hivyo kutokana na vitisho vya ndugu wa mwanamume wanaodai watamshikisha adabu kwa kuwa ameidhalilisha familia yao kushitaki suala hilo polisi wakati wangelimaliza kifamilia, anaishi kwa wasiwasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipoulizwa jana kuhusu tukio hilo, alisema hana taarifa, lakini alisema Polisi inawezekana wanafanya upelelezi ndio maana hawana jibu la moja kwa moja kwa mama huyo kiasi cha kuona anazungushwa na kumuomba aende ofisini kwake leo.
“Naomba kama anahisi anazungushwa au kuonewa, aje ofisini kwangu kesho (leo), unajua kesi kama hizi zinahitaji upelelezi, pande zote mbili lazima watafute ukweli, siwezi kusema sana maana sijafikishiwa tukio hili kwangu ila kama anaona mambo hayaendi aje,” alisema Kenyela.
Baba mzazi wa mtoto huyo alipotafutwa kwa simu ya mkononi, namba yake ilikuwa ikiita bila kupokewa na baadaye mtu mwingine alizungumza na mwandishi, kumweleza kuwa simu ya baba huyo ni mbovu.
No comments:
Post a Comment