HABARI zilizolifikia Amani muda mfupi kabla ya kwenda kiwandani zinadai kuwa sura ya mauzo kwenye filamu za Kibongo, Jacqueline Wolper Masawe aliyebadili jina na kupewa la Kiislam la Ilham, ameukacha Uislam baada ya kushindwa kukamilisha vigezo vya kuingia na kutambulika katika dini hiyo.
Na Mwandishi Wetu
Sheikh Jafaar Mohamed Fota ambaye ni Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Magomeni Kichangani ‘TIC’ aliyesimamia zoezi la kumsilimisha Wolper, hivi karibuni aliliambia Amani kuwa staa huyo tangu afikie uamuzi huo, hakurudi kukamilisha hatua za kuufikia Uislam wa kweli.
Ukamilisho aliotakiwa kuufikia Wolper kwa mujibu wa Fota ni pamoja na kuhudhuria darasa la jioni kwa siku kadhaa mfululizo, kupeleka picha tatu kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zake vizuri, mambo ambayo bidada huyo anadaiwa kushindwa kuyafanya.
Akifafanua matumizi ya picha hizo, imamu huyo alisema, moja ingetumika mahakamani kula kiapo cha kubadili jina, nyingine ni kwa ajili ya rekodi za Bakwata na msikitini.
“Cha kushangaza sasa imefika miezi mitano, sijawahi kumuona Wolper hapa,wala kusikia amefika msikiti wa wanawake kuswali, kanuni za kubadili dini hajazikamilisha, hilo ni tatizo,” alisema Fota.
Imamu huyo aliongeza kuwa, uongozi wa msikiti huo ambao ndiyo unaohusika na uamuzi wake wa kubadili dini, utamuita Wolper na kumshauri akamilishe taratibu lengo likiwa ni kumsaidia.
Kwa upande wake Wolper alipohojiwa na Amani kuhusiana na kutotimiza taratibu za Dini ya Kiislam aliyotangaza kujiunga nayo alisema: “Taratibu gani? Nimekamilisha kila kitu, mara nyingi tu nawasiliana na imamu mkuu wa msikiti huo (hakumtaja jina) ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.”
Awali staa huyo aliutangazia umma kuwa anaukacha Ukristo na kujiunga na Uislam kwa kile kilichodaiwa ni kufuata dini ya mchumba wake, Abdallah Mtoro ‘Dallas’ ambaye siku za hivi karibuni ametangaza kuuvunja uchumba wao.
No comments:
Post a Comment