Na Happiness Katabazi na Betty Kangonga.
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewahukumu adhabu
ya kunyongwa hadi kufa askari wawili wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na
mmoja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la
kumuua kwa kusudia, Swetu Fundikira.
Askari hao MT 1900 Sajenti Roda Robert (42) wa JKT, Kikosi cha
Mbweni, MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa JWTZ, Kikosi cha Kunduchi na
MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni.
Washitakiwa hao walidaiwa kumpiga na hatimaye kumuua kwa makusudi
Fundira Januari 23, majira ya saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini
Dar es Salaam na kufariki dunia usiku wa kuamkia Januari 24 mwaka 2010,
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa ajili ya
matibabu.
Sweti Fundikira ni mtoto wa mdogo wa Mwanasiasa Maarufu nchini, marehemu Chifu Abdallah Fundikira.
Hukumu hiyo ambayo inaweza kukomesha vitendo vya askari kujichukulia
sheria mkononi dhidi ya raia, ilitolewa jana na Jaji Zainabu Muruke.
Jaji Muruke alisema baada ya kusikiliza kesi hiyo, ameridhika na
ushahidi uliotolewa na mawakili wa upande wa Serikali ambao ulidai kuwa
washitakiwa walitenda kosa hilo la mauji kinyume na kifungu cha 196 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Akisoma hukumu hiyo iliyovuta hisia za wengi mahakamani hapo, Jaji
Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonesha
washtakiwa hao kuwa ndiyo waliomua marehemu (Fundikira), ushahidi
mazingira unaonesha pasipo shaka walihusika na mauaji hayo.
“Sheria ipo wazi na inaanisha kuwa ukiondoka au ukionekana na mtu kwa
mara ya mwisho na baadaye mtu huyo uliyeondoka naye akapata madhara au
amekutwa amekufa, wewe uliyeondoka naye ndiyo utawajibika kisheria na
madhara yaliyompata mtu huyo;
“Japo kuwa ushahidi uliotumiwa na upande wa mashitaka katika kesi
hii ni wa mazingira, lakini umeweza kuthibitisha kesi yao, upande wa
utetezi nao umeweza kutoa ushahidi wenye matundu mengi na unaokatika
katika sana na ambao umeshindwa kuudhoofisha ushahidi uliotolewa na
upande wa jamhuri dhidi ya washtakiwa, ’alisema jaji Mruke.
Aidha, alisema Jamhuri imeweza kuthibitisha kosa la mauaji, hivyo
mahakama imewaona washtakiwa wote wana hatia ya kumuua Swetu Fundikira.
Hata hivyo, Jaji Muruke kabla ya kutoa adhabu hiyo alimpa nafasi
wakili Karoli Muluge pamoja na washtakiwa kusema lolote kabla ya
kuwapatia adhabu hiyo.
Wakili Muluge aliiomba Mahakama iwape adhabu ndogo kutokana na
mazingira ya kesi hiyo, umri wa washtakiwa kwani bado ni vijana, nguvu
kazi ya taifa na familia zao zinawategemea.
Naye mshtakiwa wa kwanza, Sajenti Robert aliiomba Mahakama impunguzie
adhabu akidai kuwa mama yake ni mjane na anamtegemea, pia ana watoto
wadogo.
Hata hivyo Jaji Muruke alilamuamuru mshtakiwa wa pili, Koplo Ngumbe
kukaa chini baada kuanza kujitetea kuwa ametiwa hatiani kimakosa na
anamwachia Mungu.
Kwa upande wake mshtakiwa wa tatu, Koplo Rashid aliiomba mahakama
imuonee huruma na impunguzie adhabu akidai kuwa bado ni mdogo na hilo ni
kosa lake la kwanza.
Akitoa adhabu, Jaji Muruke alisema ni kweli maombi ya mshtakiwa wa
kwanza yanatia huruma na kwamba mshtakiwa wa tatu hata kumbukumbu
zinaonesha bado ni mdogo, pia hilo ni kosa lake la kwanza, lakini
alisema kuna roho iliyopotea.
“Sheria ipo wazi kabisa mshtakiwa yoyote anayepatikana na hatia adhabu
yake ni moja tu ambayo ni kunyongwa hadi kufa na hakuna mbadala wa
adhabu hiyo…hivyo mahakama hii kwa kauli moja inatamka kuwa washitakiwa
wote wa tatu mahakama hii imewahukumu adhabu ya kifo hivyo, mtanyongwa
hadi kufa,” alisema Jaji Muruke:
Baada ya kutoa adhabu hiyo Jaji Muruke alitoka katika chumba cha
mahakama na ghafla ndugu wa marehemu Fundikira waliangua vilio ndani ya
ukumbi wa mahakama, kama vile walikuwa msibani.
Ndugu wawili wa marehemu, Mwasiti Fundikira ambaye ni Dada wa marehemu
na Shelina Hamisi (mpwa wa marehemu) walianguka chini na kuzirai kwa
muda hali iliyowalazimu watumishi wa mahakama kuwapatia huduma ya kwanza
kwa kuwapepea hadi waliporejea katika hali ya kawaida.
Mke wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la Lucy ambaye aliachwa
akiwa mjamzito, alisema hakuamini kama haki ingetendeka kwani mpendwa
wao aliuwawa kinyama.
Hata hivyo wakili wa washitakiwa hao, Muluge alisema hakuridhika na hukumu hiyo na kwamba atakata rufaa.
No comments:
Post a Comment