KATIBU mkuu mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdullahman
Kinana amesema kuwa wanachama na wafuasi wa chama hicho, wasitarajie
kwamba amekuja na miujiza katika kukabiliana na matatizo yaliyomo ndani
ya chama hicho tawala.
Kinana alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu maswali katika kipindi
cha Jenerali On Mondey, kinachoongozwa na mwandishi wa habari nguli,
Jenerali Ulimwengu, na kurushwa na kituo cha televisheni cha DTV cha
jijini Dar es Salaam.
Alisema tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu, amekuwa akipata salamu nyingi
za pongezi kutoka kwa wanachama wa kada mbalimbali, wakiwemo waliokata
tamaa na kumwambia sasa wanarudi kwenye chama baada ya yeye kushika
nafasi hiyo.
“Wapo wanachama wengi waliokata tamaa na hata wale waliohamia
upinzani, wamenipigia na kunipa pongezi na kusema kwamba sasa wako
tayari kurudi CCM na wana matarajio makubwa sana kutoka kwangu.
Mimi nawaambia wasitarajie miujiza kwamba nimekuja na dawa ya matatizo
yote ya CCM, lakini nawahakikishia nitasimamia utekelezaji wa maamuzi
yote ya chama,” alisema Kinana.
Kada huyo maarufu ndani ya CCM alisisitiza kuwa hajaja na miujiza bali
ataongoza kwa kufuata katiba na kubwa kuliko yote ni kusimamia
utekelezaji wa maazimio ya vikao vya chama.
Akitolea mfano wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliomalizika hivi
karibuni, Kinana alisema atahakikisha anasimamia utekelezaji wake.
Baadhi ya maazimio ya mkutano huo uliomalizika wiki iliyopita mjini
Dodoma ni pamoja na kuitaka Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kuendelea na
zoezi la kuwabaini na kuwaondoa viongozi na watendaji wa chama
wanaoenda kinyume na maadili ya viongozi-wanaokipaka chama matope.
Mkutano Mkuu huo, pia uliiagiza serikali kuwachukulia hatua kali na za
haraka viongozi na watendaji wa serikali ambao ni wala rushwa,
wabadhirifu na wanaotumia vibaya madaraka yao.
Katika kushughulia nidhamu na uwajibikaji wa viongozi wa chama, Makamu
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula, alisema juzi kuwa hawatasubiri
uamuzi wa mahakama katika kushughulikia wala rushwa na mafisadi kwani
chama kinaweza kuchukua hatua zake mara moja.
Sifa moja kubwa anayotajwa kuwa nayo Kinana ni msimamo mkali dhidi ya
masuala ya ufisadi na kubwa zaidi anatajwa kuwa bingwa wa mikakati ya
kisiasa ndani ya chama hicho.
Kinana ndiye aliyeongoza kampeni za Benjamin Mkapa mwaka 1995, dhidi
ya Augustine Mrema, aliyekuwa mwanasiasa maarufu na aliyekubalika kwa
wakati huo.
Tangu wakati huo, Kinana amekuwa akiongoza kampeni za urais na mtu
anayependa kusimamia mawazo anayoamini ni sahihi, lakini akiwa tayari
kuunga mkono hoja zenye lengo la kukijenga chama hicho.
Kuhusu kudhibiti makundi yanayotaka urais ambayo yamesababisha mpasuko
mkubwa ndani ya chama, Kinana alisema uongozi mpya utadhibiti kasi ya
wagombea na kwa sasa inawataka waache kuwapotezea wananchi muda kwa
kufikiria urais mwaka 2015 badala ya kufikiria maendeleo.
“Kuna mambo mengi ya kufikiria kwa sasa hasa masuala ya uchumi na
namna ya kuwakwamua wananchi kiuchumi, muda wa urais haujafika na
wanaotaka kugombea wasubiri hadi Mei 2015,” alisema Kinana.
Katibu Mkuu huyo aliyerithi mikoba ya Wilson Mukama aliwataka wana CCM
kushirikiana na kuvunja makundi hasa baada ya uchaguzi wa ndani
kumalizika.
Pia alisema kuanzia leo, viongozi wapya wa sekretarieti wataanza
kufanya ziara mikoani kuhimiza na kuimarisha uhai wa chama hicho ambacho
katika siku za hivi karibuni, kimepoteza mvuto.
No comments:
Post a Comment