MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), kwa sasa ndiye
anashikilia rekodi ya ukinara wa kuchangia mara nyingi bungeni kwa mwaka
2012, akifuatiwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA)
na Godfrey Zambi wa Mbozi Mashariki (CCM).
Kwa mujibu ya rekodi zalizomo kwenye mtandao wa Bunge, Mnyika ambaye
ni kipindi chake cha kwanza bungeni, ameonekana kufanya vizuri zaidi
sambamba na wabunge wenzake kadhaa wa CHADEMA.
Takwimu hizo hazijawahusisha mawaziri, manaibu wao, Spika, naibu wake,
wenyeviti watatu wa Bunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa vile nafasi zao zinawapa uwezekano
mkubwa wa kuchangia hoja wakati wowote.
Wabunge kumi ambao wameshika nafasi za juu ni Mnyika akiwa amechangia
mara 184, kuuliza maswali ya nyongeza 28 na ya msingi 7, akifuatiwa na
Zitto (mchango 79, maswali ya nyongeza 25 na maswali ya msingi 8) wakati
Zambi anashika nafasi ya tatu kwa kuchangia mara 70, (maswali nyongeza
26) na (maswali ya msingi 9).
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anashika nafasi ya nne akiwa
amechangia mara 93, maswali ya nyongeza 19 na yale ya msingi 7,
akifuatiwa na Diana Chilolo wa Viti Maalumu (CCM) aliyechangia mara 61,
maswali ya nyongeza 41 na msingi 9.
Nafasi ya sita inashikiliwa na Halima Mdee wa Kawe (CHADEMA) akiwa na
rekodi ya michango 59, maswali ya nyongeza 15 na ya msingi 6 akifuatiwa
na Moses Machali wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi) mwenye michango 57,
nyongeza 30 na maswali ya msingi 7.
Magdalena Sakaya wa Viti Maalumu (CUF) ameshika nafasi ya nane akiwa
na michango 52, maswali ya nyongeza 13 na ya msingi 4, huku Mbunge wa
Kisarawe, Seleman Jafo (CCM) akifuatia kwa michango 51, maswali nyongeza
10 na ya msingi 6.
Anayefunga dimba kwa kumi bora ni Ester Bulaya wa Viti Maalumu (CCM)
mwenye michango 47, maswali ya nyongeza 17 na maswali ya msingi 3, akiwa
amefungana na Martha Mlata wa Viti Maalumu (CCM) mwenye rekodi ya
michango 47, maswali ya nyongeza 11 na ya msingi 5.
Ni takriban miaka miwili tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, ambapo
vyama vya upinzani hususan CHADEMA, wabunge wake wameendelea kuonesha
umahiri bungeni.
Hata Bunge la tisa lililopita kwa mujibu wa utafiti wa shirika moja,
Zitto na Dk. Willibrod Slaa akiwa mbunge wa Karatu wakati huo, walishika
nafasi za juu.
Katika mtiririko huo wa takwimu hizo kwenye mtandao wa Bunge, wabunge
wanaoonekana kuwa na alama ndogo wengi ni wale wa Viti Maalumu CCM na
baadhi wa CUF.
No comments:
Post a Comment