Na na Joachim Mushi, Korogwe
BAADHI ya wanafunzi waliofanya mitihani wa mchujo wa kidato cha
pili katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe huenda wakazuiliwa kupewa
matokeo yao kutokana na kutokuwa na fomu namba 9 (TSM9) za usajili
katika shule zao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi wilayani Korogwe, na
kuthibitishwa na Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wilaya hiyo, miongoni mwa
wanafunzi ambao wataathirika na tatizo hilo ni kutoka katika shule za
sekondari Bungu, Patema na Mfundia.
Taarifa zinaeleza wanafunzi hao walifanya mitihani yao bila ya kuwa na
fomu hizo, hivyo walimu wakuu wa shule husika kuamriwa wawasilishe namba
za wanafunzi hao katika kituo cha kusahihishia mitihani hiyo.
Akizungumzia tatizo hilo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya
Wilaya ya Korogwe, Shaban Shemzighwa, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na
kudai walipokea malalamiko ya baadhi ya wanafunzi juu ya utata huo.
Hata hivyo, alisema wanafunzi waliokuwa na utata juu ya suala hilo
waliruhusiwa kufanya mitihani na baadaye walimu wakuu wa shule zao
kutakiwa kuwasilisha namba za wanafunzi hao.
Jumla ya wanafunzi wa kidato cha pili 442,925 walifanya mitihani ya mchujo wa kidato hicho Novemba 5, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment