Rais Mohammed Mursi wa Misri siku ya jana amefanya ziara hapa Ujerumani ambapo
amekutana na Kansela Angela Merkel. Mursi alipokelewa kwa gwaride la
heshima katika ofisi ya Kansela.Wanajeshi walikuwa wamejipanga nje ya ofisi ya Kansela Merkel mjini
Berlin, kumpokea rais Mohammed Mursi.
Merkel na mgeni wake walitembea
katika zulia jekundu huku tarumbeta zikiburudisha. Hii ni mara yake ya
kwanza kwa Mursi kuitembelea Ujerumani. Baada ya kula chakula cha mchana
pamoja, Merkel na Mursi walizungumza na waandishi wa habari.
Awali Mursi alikuwa amepanga kubakia Berlin kwa muda wa siku mbili
lakini hali tete ya usalama nchini mwake imemlazimisha kurejea nyumbani
leo. Alikuwa amedhamiria pia kuitembelea Ufaransa siku ya Ijumaa, lakini
safari hiyo imebidi ifutwe.
Mvua ilikuwa inanyesha wakati Merkel na Mursi walipoelekea katika ofisi ya Kansela
Akizungumza na waandishi wa habari, Kansela Merkel alisema
kwamba anataka kuona mazungumzo yakifanyika na vyama vyote vya kisiasa.
Pamoja na hayo ameitaka serikali ya Mursi iheshimu haki za binadamu.
Masuala ya kiuchumi yalizungumziwa pia. "Kwa mtazamo wangu, ukuaji wa
kiuchumi ni jambo linalowawezesha wananchi kuwa na maisha mazuri. Ni
muhimu mgogoro wa uchumi uepukwe. Kwa njia hiyo uchumi utasaidia pia
kuimarisha hali ya kisiasa."
Mbali na mgogoro wa kisiasa unaoendelea, tatizo kubwa linaloikabili
Misri kwa sasa ni la kiuchumi. Idadi ya watalii imepungua kwa kiasi
kikubwa baada ya mapinduzi kutokea mwaka 2011. Hivi sasa Misri inahitaji
wawekezaji kutoka nje. Hapa Ujerumani, wafanyabiashara wanaelewa kwamba
Misri ni mahala pazuri pa kuwekeza lakini wanahofia hali ya usalama.
Mursi aahidi demokrasia zaidi
Maandamano yaliyoambatana na vurugu katika uwanja wa Tahrir.
Nchini Misri kwenyewe viongozi wa vyama vya upinzani
wametangaza kuwa tayari kufanya mazungumzo na serikali. Mohammed El
Baradei ambaye ni kiongozi katika chama cha ukombozi wa kitaifa ametoa
tangazo hilo siku mbili tu baada ya upinzani kusema kwamba hauko tayari
kwa mazungumzo.
Katika mkutano wake na Kansela Merkel, rais Mursi ameahidi kuharakisha
juhudi za kuleta demokrasia nchini mwake, akisema kuwa Misri inataka
kuwa nchi inayofutata utawala wa sheria. "Misri itakuwa nchi inayoruhusu
uhuru wa kutoa maoni," alieleza Mursi akiishukuru Ujerumani kwa kuwa
mshirika wake katika juhudi za kuleta demokrasia.
Kiongozi huyo ametaja pia kwamba yuko tayari kupanua mahusiano baina ya
nchi yake na Ujerumani lakini akasisitiza kwamba ushirikiano huo
hautakiwi kuwa kigezo cha nchi moja kuingilia mambo ya ndani ya nchi
nyingine. Mursi anakutana pia na wawakilishi wa sekta mbali mbali za
kiuchumi hapa Ujerumani kutafuta wawekezaji.
No comments:
Post a Comment