Shirika la Maripota wasiokuwa na Mipaka limechapisha ripoti yake kuhusu
uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2012.Barani Afrika Somalia inatajwa
kuwa nchi hatari zaidi kwa waandishi habari.
Ripoti ya Maripota wasiokuwa na mipaka inaitaja Somalia kama mahala
hatari kabisa kwa waandishi habari mnamo mwaka 2012 : waandishi habari
18 waliouliwa nchini humo,naiwe kwa kujikuta mahala mabomu yalikokuwa
yanaripuliwa au kwa kulengwa makusudi na wauwaji .Taifa hilo la pembe ya
Afrika limeorodheshwa nafasi ya pili ya nchi hatari kwa waandishi
habari baada ya Syria.
Nchini Eritrea,inayoburura mkia pia katika orodha
hiyo kwa mwaka wa sita mfululizo,hakuna mwandishi habari aliyeuliwa
lakini kuna baadhi walioachwa jela hadi kufa.Kuna waandishi habari
wasiopungua 30 korokoroni nchini humo hali inayoifanya nchi hiyo
iangaliwe kama jela kubwa kabisa ya waandishi habari barani Afrika.Kati
ya wafungwa 11 wanaoshikiliwa jela tangu mwaka 2001,sabaa wameshafariki
dunia kutoana na hali mbaya katika jela hizo au kwa kujiuwa wenyewe.
Afrika Mashariki pia inaangaliwa kama eneo la mchujo wa habari na
kuandamwa waandishi habari.Sudan ya Omar al Bashir ambako magazeti
yanazidi kufungwa na kamata kamata ya waandishi habari kuendelea msimu
wa kiangazi,inashikilia nafasi ya 170 mkiani,huku Djibuti ambayo pia
haina vyombo huru vya habari na inayomshikilia ripota wa kituo cha
matangazo cha La Voix de Djibuti,ikikamata nafasi ya 167.
Licha ya
kuachiwa huru waandishi habari wawwili wa kutoka Sweden,Ethiopia
inakamata nafasi ya 137 kutokana na sheria zake za ukandamizaji
zilizopitishwa mwaka 2009 na kwasababu ya kuendelea kuwashikilia
kizuwizini baadhi ya waandishi habari wa kienyeji.
Tanzania imeangukia nafasi ya 70
Christian Mihr , mwenyekiti wa shirika la Maripota wasiokuwa na mipaka nchini Ujerumani
Christoph Dreyer wa shirika la Maripota wasiokuwa na mipaka kutoka
Berlin anachambua hali ya mambo akisema:"Afrika mashariki hali ni
tofauti.Maendeleo mabaya yameripotiwa Tanzania nchi ambayo hadi sasa
ilikuwa ikisifiwa sana.Lakini katika mwaka 2012 imepoteza nafasi 36 na
kuteleza hadi nafasi ya 70 kutokana na vifo viwili vya waandishi
habari.Mmoja alikutikana amekufa,yadhihirika ameuliwa na mwengine
ameuwawa wakati wa maandamano.Hii si hali nzuri kwa vyombo vya habari."
Wimbi la mageuzi halikuzisaidia sana nchi za kiarabu
Nembo ya Maripota wasiokuwa na Mipaka-tawi la Ujerumani
Miaka miwili baada ya wimbi la mageuzi katika nchi za kiarabu uhuru wa
vyombo vya habari bado ni tete katika nchi nyingi ikiwa ni pamoja na
Misri ambako waandishi habari na wanablogi bado waaendelea kuhujumuiwa
,kukamatwa na kufikishwa mahakamani.Nchini Tunisia waandishi habari
wanazidi kushambuliwa na serikali inakawia kutia njiani sheria mpya
kuhusu vyombo vya habari.Libya baada ya kung'olewa madarakani utawala wa
muammar Gaddafi inaonyekana kufanya vyema na kuchupa nafasi 23 hadi
kuifikia nafasi ya 131.
Miongoni mwa nchi za Ulaya, Ujerumani inashikilia nafasi ya 17: Tatizo
hapa linatokana na ukosefu wa fedha uliosababisha baaadhi ya vyombo vya
habari kufungwa.Sababu nyengine inatokana na ile hali kwamba wajasiria
mali uwekeza katika vyombo vya habari ili kuweza kuwa na usemi katika
kile kinachoandikwa.
CHANZO CHA HABARI NA DW
No comments:
Post a Comment