NI wazi sasa sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, huenda
likawa limefifia bila Jeshi la Polisi kulifanyia kazi kwa kina ikiwemo
kumhoji majeruhi huyo.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26 mwaka jana, na kuteswa,
kuumizwa vibaya ikiwa ni pamoja na kung’olewa kucha na meno kisha
kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam
na watu wasiojulikana zikiwa ni siku chache tangu kuanza kwa mgomo wa
madaktari.
Hata hivyo, kutokana na utata wa tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam chini ya Kamanda wake, Suleiman Kova, liliunda
tume ya wataalam kutoka ndani ya jeshi iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi
ili kuchunguza sakata hilo lilikokuwa likihusishwa na serikali.
Hatua hiyo ilikuja kutokana na Dk. Ulimboka kuwataja baadhi ya watu
aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini mpaka sasa licha
ya mtu mmoja raia wa Kenya, Joshua Mulundi, kufikishwa mahakamani
akituhumiwa kuhusika na tukio hilo, watuhumiwa wengine hawajawahi
kuhojiwa.
Tume hiyo hata hivyo, haikuwahi kutoa ripoti yake kama Kova
alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka
hajawahi kuhojiwa huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana
na sakata hilo.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, jeshi hilo kupitia kwa msemaji
wake, Advera Senso, jana limekanusha kuwepo kwa tume hiyo akisema kuwa
walioteuliwa ni polisi ambao watafanya kazi za kiuchunguzi kwa
taratibu za jeshi hilo.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, ambaye alikiri kuwepo kwa
tume hiyo, lakini akasema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa vile
taarifa zake alishazipeleka kwa wakubwa wake makao makuu baada ya
kukamilisha wajibu wake.
“Hili suala lipo mahakamani kwanza, na kuhusu kuhojiwa au kutokuhojiwa
kwa Dk. Ulimboka hilo lipo kwa mkubwa wangu, sasa unataka mimi niseme
kama amehojiwa au la wakati sijui kinachoendelea huko?” alisema Kova.
Lakini Senso aliliambia Tanzania Daima kuwa, hakukuwepo na tume hiyo
na kwamba walioteuliwa ni polisi ambao walifanya kazi za kiuchunguzi
kwa taratibu za jeshi hilo.
Alisema Jeshi la Polisi lisingeweza kuunda tume katika suala zima la
Dk. Ulimboka kwa kuwa kilichotokea ni uhalifu kama uhalifu mwingine, na
litashughulikiwa kwa mujibu wa jeshi hilo.
“Kwanza hilo ni suala la mwaka jana na sisi ripoti za mwaka huo
tumeshafunga, labda nianze kufuatilia sasa hivi kujua limefikia wapi,”
alisema Senso.
Alipoulizwa wao kama Jamhuri wanaendeshaje kesi hiyo ikiwa shahidi wa
kwanza, Dk. Ulimboka hajachukua maelezo yake, Senso alisema kuwa
daktari huyo anaweza kupeleka malalamiko yake kwao ili waweze
kuyafanyia kazi.
Aliongeza kuwa, wakati polisi wakiendelea na uchunguzi, mlalamikaji
anaweza kwenda kwao kutoa taarifa anazozijua kwa ajili ya kusaidia
uchunguzi huo.
Alipotakiwa kuelezea kama walishawahi kumfuatilia Ramadhan Ighondu
(Abeid) aliyetajwa na Dk. Ulimboka kuhusika na utekwaji wake, Senso
alisema akiwa kama msemaji wa jeshi ana mipaka ya kuzungumzia suala
hilo kwa ajili ya kutokuingilia kesi iliyopo mahakamani.
“Hatuwezi kila jambo tukawa tunalitangaza hadharani kuwa tumefanya
hivi, tumefanya hivi, na mkumbuke ninyi ni waandishi wa habari peke
yake, lakini mimi ni mwanahabari na askari vile vile,” alitamba.
Wakati vigogo hao wakisigana katika kulifafanua sakata hilo, Dk.
Ulimboka mara kadhaa amekuwa akieleza kuwa yupo tayari kutoa maelezo
yake kama kutakuwa na tume huru ambayo si hiyo iliyoundwa na polisi
wenyewe.
Katika tamko lake mwishoni mwa mwaka jana lililosomwa kwa niaba yake
na wakili wa kujitegemea, Nanyooro Kicheere, akimwakilisha mwanasheria
wake, Dk. Ulimboka, alisema wapo watu ambao hawatapenda kusikia siri
iliyojificha katika tukio zima la kutekwa kwake na kwamba hana jinsi
zaidi ya kueleza ukweli.
Alisema kuwa tukio la kutekwa kwake, kusukumizwa kwenye gari,
kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno;
na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande, lilitokea wakati akiwa
kikao na ofisa aliyetambulishwa kwake ni ofisa wa Ikulu, Ramadhani
Abeid Ighondu.
Aidha, Dk. Ulimboka alisema hata namba za simu zilizokuja kutambulika
baadae kuwa zilikuwa zikitumiwa na Ighondu ndizo hizo alizokuwa
akitumia mtu aliyejifahamisha kwa jina la Abeid kutoka Ikulu.
Alisema anamfahamu Abeid (Ighondu) na kwamba hata akikamatwa
atakwenda kufanya utambuzi, na kwamba anasikitishwa hadi wakati huo wa
kutoa taarifa yake kuwa mtu huyo hajakamatwa, wala hakuna
kinachoendelea juu yake.
Chanzo cha habari Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment