WANACHAMA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kata
ya Gongo la Mboto Dar es Salaam, wamemtaka diwani wa kata hiyo ambaye
pia ni Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, kutoa ufafanuzi kuhusu
kiasi cha sh milioni 100 kilichotengwa kwa ajili ya matengezo ya
barabara katika bajeti ya 2011/2012.
Akizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wanachama
hao, Katibu wa Jimbo la Ukonga, Juma Mwaipopo, alieleza kuwa fedha hizo
zilitengwa na Halmashauri ya Ilala katika kipindi hicho ambazo hadi sasa
hazijafahamika zilikokwenda.
Alifafanua kuwa katika bajeti hiyo halmashauri ilitenga sh bilioni 93
kwa matumizi ya jimbo hilo, zikiwemo sh milioni 100 kwa kata sita
zilizo Gongo la Mboto ambazo zingetumika kwa ajili ya upanuzi na
matengenezo ya barabara pamoja na kusambaza huduma ya maji kwa wananchi,
jambo ambalo hadi sasa ni kitendawili.
Alisema bado tatizo la huduma ya maji safi katika kata hiyo ni
kitendawili ambacho kimeshindikana kupatiwa ufumbuzi na serikali.
“Tunahitaji kuwa na maamuzi ya pamoja juu ya Silaa, kwa sababu hatujui
tumetoka wala tunaelekea wapi hadi sasa? Inawezekana hajui kazi yake
kwa sababu hatuna maendeleo wala mabadiliko katika kata yetu, Watanzania
tudai haki ambazo serikali ilituahidi itazitekeleza bure,” alisema
Mwaipopo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CHADEMA), Ezekia Wenje, alitumia
fursa hiyo kueleza kuwa diwani huyo ameshindwa kutekeleza majukumu yake
hasa kwa kushindwa kukutana na wananchi wake walau kwa mwaka mara moja
ili kutoa ufafanuzi juu ya mapato na matumizi ya fedha yanavyotumika.
Alipopigiwa simu kujibu tuhuma hizo diwani huyo alikata na kutuma
ujumbe mfupi wa maneno: “Niko sehemu tata; naomba unitumie ujumbe wa
maneno (sms).”
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment