WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), amepanga kutoa vyeti vingi vya kuzaliwa kwa wananchi ndani ya mwaka 2013.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Phillip Saliboko, katika taarifa yake ya salamu za Mwaka Mpya.
Saliboko amewataka wananchi kufika katika ofisi za wakala huyo ili
kupata huduma hiyo ambayo imeboreshwa na kwa kipindi kifupi unapata
cheti tofauti na ilivyokuwa awali.
“RITA tunatoa huduma zipatazo 17 kwa wananchi kubwa likiwa ni usajili
wa vizazi na vifo ambao hupatikana makao makuu na katika wilaya zote
nchini…kimsingi tumejitahidi kwa mwaka uliopita kuwahudumia wananchi
wetu vizuri na tunaahidi kufanya maboresho ili kuweza kuwafikia wananchi
wengi zaidi,” alisema.
Alisema moja ya mikakati yao ni kufanya kampeni za usajili na kutoa
vyeti vya kuzaliwa katika wilaya 12 huku wakipita kila kata za wilaya
ambazo zitachaguliwa hatua itakayosaidia wananchi wengi zaidi hasa wa
maeneo ya vijijini kupata vyeti hivyo.
“Tunawashukuru viongozi wote katika wilaya tulizofanya kampeni kwa
ushirikiano mkubwa waliotupatia na kufanikisha mikakati hii na kwa mwaka
mpya wa 2013 tunakusudia kuimarisha mpango huu na kuutekeleza katika
wilaya nyingi zaidi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema
Saliboko.
Saliboko alisema kuwa mkakati mwingine ni pamoja na kuanza kusajili
watoto walio na umri chini ya miaka mitano (Under Five Birth
Registration Initiative – U5BRI) ambao utekelezaji rasmi unategemewa
kuanza mkoani Mbeya Aprili mwaka huu.
Alisema kuwa katika mkakati huu watoto walio na umri huo watasajiliwa
na kupata vyeti vya kuzaliwa bila malipo katika ofisi za watendaji kata
na katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya afya ya mtoto.
Saliboko alisema kuwa RITA inategemea pia kutoa huduma za usajili
katika taasisi na mashirika na kuzipa uwezo zaidi ofisi zake za wilaya
katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za wakala.
No comments:
Post a Comment