MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD), umedai 
kupokea kwa mshangao taarifa zilizoandikwa na gazeti la serikali 
zikisema kuwa Rais Jakaya Kikwete amelizika rasmi gazeti la MwanaHalisi 
kwa uchochezi.

Kwamba habari hiyo imeupotosha umma kwa kiwango kikubwa, na hivyo 
wanaitaka 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kutoa ufafanuzi, 
kutokana na kupotoshwa kwa kosa lililosababisha gazeti hilo kufungiwa.
Mtandao huo ambao ni mkusanyiko wa mashirika zaidi ya 60 ya watetezi 
wa haki za binadamu wakiwamo wanasheria, waandishi na watetezi wengine, 
ulisema kuwa habari hizo ni za upotoshaji kwa sababu zinamkariri Rais 
Kikwete akiwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Kwamba habari iliyochapishwa na gazeti hilo la HabariLeo ilidai kuwa 
MwanaHalisi lilifungiwa kwa sababu liliandika habari ya uchochezi 
ikiwataka askari kuasi na kutotii amri.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mratibu wa Mtandao huo, 
Onesmo Olengurumwa alisema kuwa habari hiyo haikuandikwa na gazeti la 
MwanaHalisi bali gazeti jingine ambapo tayari watuhumiwa wamefikishwa 
mahakamani.
“Tunaamini kilichoandikwa na mwandishi wa gazeti hilo ndiyo kauli 
iliyotolewa na Rais Kikwete kwa sababu habari hiyo imeletwa na mhariri 
mzoefu na makini, na tunaamini hivyo kwa sababu rais ameitoa kauli hiyo 
mahali pake, wakati akiwasilisha ripoti ya Tathmini ya Utawala Bora 
(APRM),” alisema.
Aliongeza kuwa, wanashawishika kuamini kwamba iwapo siku zote Rais 
Kikwete alikuwa akiamini kuwa MwanaHalisi ndiyo waliochapisha habari 
inayohusu askari kugoma, basi alipotoshwa tangu mwanzo na hivyo 
anahitaji kuelimishwa vizuri juu ya suala hilo.
  Alisisitiza kuwa, wanaendelea kuamini kuwa MwanaHalisi lilionewa kama 
sababu zilizosababishwa kufungiwa ni pamoja na zile ambazo gazeti hilo 
lilimnukuu Rais Kikwete huko Ethiopia.
  Katika habari hiyo, Rais Kikwete alikaririwa akisema “...Ndio kuna 
gazeti moja tumelifungia na kuna watu wanaosema tuliondolee 
adhabu…tumesema hapana…kutaka Jeshi liasi huu sio uandishi wa habari.”
MwanaHalisi lilifungiwa na serikali Julai 30 mwaka jana, kutokana na 
habari yake iliyomhusisha ofisa wa Ikulu katika sakata la kutekwa na 
kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, 
kudaiwa kuwa ni ya uchochezi.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers (HHPL) 
inayochapisha MwanaHalisi, Saed Kubenea, alipoulizwa juu ya kauli ya 
rais, alisema ameipokea kwa faraja.
  “Tuna taarifa za serikali kukamata na kushitaki mwandishi aliyeandika 
habari ambazo serikali ilisema zinachochea uasi katika majeshi; mhariri 
wa gazeti lililozichapisha na mwenye mtambo uliochapa gazeti. Lakini 
hayo yote hayahusu MwanaHalisi,” alisema.
  Alisema kuwa kwake si gazeti wala waandishi wa habari wanaotuhumiwa 
uchochezi wa jeshi. Lakini kama walifungiwa kwa madai hayo, basi sasa 
rais ameibuka na ukweli ambao utawaweka huru.
                                           CHANZO TANZANIA DAIMA 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment