HATIMAYE msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, jana
alipata dhamana baada ya kutimiza masharti matano aliyopewa na Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, juzi.
Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msainii mwenzake Steven Kanumba.
Lulu alitimiza masharti hayo jana saa 9 alasiri kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Francis Kabwe.
Baada ya kutimiza masharti hayo ya dhamana, aliwaeleza waandishi wa
habari huku akitokwa machozi kuwa anamshukuru Mungu, kwani yeye ndiye
alifanya akapata dhamana hiyo na hivyo kumfanya atoke gerezani na
kurejea kuishi uraiani.
Lulu ambaye alikuwa ameongozana na wakili wake Peter Kibatara, alisema
anawashukuru wale wote waliokuwa naye bega kwa bega, tangu kesi yake
ilipoanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
“Ninachoweza kusema ni kuwashukuru wale wote waliokuwa wakinihangaikia
na kuniombea kwa Mungu hadi leo nimepata dhamana, narudi kuungana na
familia yangu…lakini naomba watu hao waendelee kuniombea, kwani leo
nimepata dhamana tu na ile kesi yangu ya msingi ya kuua bila kukusudia
bado haijaanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi, hivyo naombeni sana
waendelee kuniombea na wasinitupe,” alisema Lulu.
Msanii huyo amedhaminiwa na Florian Matungwa, ambaye anatoka Wizara ya Ardhi na Verus Mboneko Wizara ya Afya.
Lulu alifikishwa eneo la Mahakama Kuu saa 7:58 mchana na gari ya Jeshi
la Magereza lenye namba za usajili STK 2823. Baada ya kupatiwa dhamana,
aliondoka na gari aina ya Land Cruiser VX V8, lenye namba za usajili
T480 CFX.
Hata hivyo, Wakili Kibatara, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kwa
niaba ya mteja wake, anakanusha uvumi uliokuwa umeenea kuwa Lulu
angeliachiwa kwa dhamana jana angeenda moja kwa moja kwenye kaburi
alilozikwa Kanumba lililoko eneo la Kinondoni na kuongeza kwa kumshukuru
Msajili Kabwe, kwa kumpatia dhamana mteja wake, kwani muda wa kazi
ulikuwa umepita.
Mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence
Massawe waliiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye
amesota rumande katika gereza la Segerea tangu Aprili mwaka jana, ambapo
walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha
148(1), (2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2002 .
Jaji Mruke alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe
kwa Msajili wa Mahakama hiyo hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es
Salaam bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi, kuwa
na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali ambao watasaini
bondi ya sh milioni 20 kila mmoja.
Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo, Lulu alishindwa kupata
dhamana hiyo baada ya Msajili wa Mahakama kutokuwepo ofisini hiyo juzi.
Wasanii waliokuwepo kumuunga mkono Lulu mbali na mama yake mzazi
mahakamani hapo, ni Mahsein Awadh maarufu Dk. Cheni, Muna na msanii
mwingine ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
No comments:
Post a Comment