SERIKALI imeahidi kuanza kutafakari juu ya suala la makampuni ya
 simu ambayo hayataki kupeleka huduma hiyo katika maeneo yote ambayo 
hayana mawasiliano ya simu kwa kuwapunguzia masafa.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa 
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba wakati alipokuwa 
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba 
(CCM) aliyetaka kujua mpango wa serikali katika kuyalazimisha makampuni 
hayo ya simu kupeleka huduma hiyo katika maeneo yasiyo na simu.
“Serikali itaanza kutafakari suala hili kwa kina ikiwa ni pamoja na 
kuwanyang’anya ama kuwapunguzia masafa makampuni haya ya simu katika 
maeneo yote ya hapa nchini yasiyo na umeme,” alisisitiza Makamba.
Katika swali lake mbunge huyo alihoji kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfuko 
wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) bado kumekuwepo na ahadi nyingi toka 
serikalini kuwa, wanafanya upembuzi yakinifu, wapo katika mchakato, 
lakini hadi sasa hakuna hata mnara mmoja uliojengwa katika maeneo ambayo
 hayana umeme, hususani kwa Jimbo la Manyovu na hivyo kutaka kauli ya 
serikali.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Manyovu, Albert Ntabaliba (CCM) 
alitaka kujua ni lini Tarafa ya Muyama katika Jimbo la Manyovu itawekewa
 mnara wa mawasiliano, na lini serikali itafika Manyovu kuona hali 
ilivyo, ikilinganishwa na minara iliyopo upande wa Burundi wakati upande
 wa Tanzania hakuna minara.
  Akijibu swali hilo, Makamba alisema serikali kupitia UCAF tayari 
imekwishachagua kampuni ya simu itakayopeleka mawasiliano katika Tarafa 
ya Muyama.
  Alibainisha kuwa wizara yake imetenga ruzuku ya jumla ya dola za 
Kimarekani 173,000 kwa ajili hiyo na kwamba kazi hiyo inatarajiwa kuanza
 kabla ya Machi mwaka huu.
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment