HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, imelipa
fidia ya sh milioni 186 kwa wamiliki wa nyumba tisa katika eneo la
Ubungo Kibangu kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara itakayounganisha
wakazi wa Kimara Makoka na maeneo mengine ya jiji.
Akizungumza katika eneo la Ubungo Kibangu, juzi alipokwenda kukagua
utekelezaji wa kuvunjwa kwa nyumba hizo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni,
Yusuph Mwenda, alisema taratibu za ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu
wa kilometa 3.5 utaanza leo chini ya mkandarasi, Gwemah Decoreta Company
Limited, na utakamilika baada ya miezi mitatu.
Mwenda alisema barabara hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha Changarawe
itagharimu sh milioni 300 ambazo zimetolewa na manispaa kupitia kodi
mbalimbali zinazokusanywa.
“Hizi shilingi milioni 186 ni kodi ya Watanzania zilizokusanywa na
manispaa ya Kinondoni. Leo zimelipa fidia hapa kama kusingekuwa na
ulipaji fidia tungefanyia maendeleo mengine kwa ajili ya manispaa yetu,
hivyo ni wakati wa kujifunza namna ya kuweka miji katika mpangilio mzuri
utakaoepusha gharama kama hizi,” alisema Mwenda.
Alisema lengo la kutengeneza barabara hiyo ni kupunguza foleni kwa
wakazi wa Kimara na maeneo mengine ya jirani ambao kwa sasa wanalazimika
kutumia barabara ya Morogoro.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Manispaa ya
Kinondoni, Tarimba Abbas, alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutaondoa
dhana iliyojengeka miongoni mwa watu kuwa maeneo yanayoongozwa na vyama
vya upinzani serikali haitaki kuboresha miundombinu.
No comments:
Post a Comment