JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia askari wawili kutoka
mkoani Kagera pamoja na raia wawili baada ya kukutwa na vipande 17 vya
meno ya tembo.
Akizungunza na Tanzania Daima, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom
Mwakyoma, alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana
saa nane katika Kijiji cha Lwamchanga, Tarafa ya Logoro wilayani
Serengeti.
Mwakyoma alisema kuwa siku hiyo, askari waliokuwa doria, kwa
kushirikiana na askari wa kikosi cha wanyama pori, waliwakamata watu
wawili, Boniface Kurwa (31) mkazi wa Geita akiwa na pikipiki yenye namba
za usajili T 874 CCC aina ya Sunlg akiwa na mwenzake Nyarata mkazi wa
mjini Mugumu ambaye pia alikuwa na pikipiki namba T 834 ZPH aina ya
Toyo.
Alisema kuwa baada ya kusimamishwa na askari hao, walitupa pikipiki na
kukimbia, lakini Kurwa alikamatwa, na pikipiki zao zilipokaguliwa
zilikutwa zimepakia vipande 17 vya meno ya tembo.
Kamanda alisema kwa idadi ya meno hayo, ni sawa na tembo watatu
wameuawa na kwamba baada ya kukamatwa, Kurwa alitoa ushirikiano akidai
kuwa waliowatuma pembe hizo wapo katika hoteli moja iitwayo Garakisi ya
mjini Mugumu.
Aliongeza kuwa walikwenda na kuwakuta askari wawili mmoja mwenye namba
E 9172 D/C, Koplo David ambaye ni wa Kituo cha Polisi Biharamulo na F
5553 D/C Jerad wa Kitengo cha
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bukoba.
“Baada ya kuhojiwa, askari hao walikiri kuwa wamefika huko baada ya
kuelekezwa na mtu mmoja aitwaye Boniface Emmanuel maarufu kama
Mnyarwanda ambaye ni mkazi wa huko Biharamulo,’’ alisema.
Kamanda alisema kuwa askari hao walikuwa na gari dogo lenye namba za
usajili T 403 BTK aina ya Carina mali ya D/C Jerad ambalo pia
limeshikiliwa na polisi, huku watuhumiwa wote wakitarajiwa kufikishwa
mahakamani muda wowote upelelezi utakapokamilika.
Chanzo cha habari na Berensi Alikadi, Musoma-Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment