RAIS Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya waombolezaji
pamoja na marais wastaafu wa Tanzania kwenye mazishi ya Askofu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini
Kati, Dk. Thomas Laizer, na kumtaja kama kiongozi jasiri na jabali
lililoiletea dayosisi hiyo maendeleo makubwa.
Viongozi wengine watakaoshiriki mazishi hayo yaliyofanyika katika eneo
lililotengwa katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri usharika wa Mjini
Kati ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais
mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu aliayejiuzulu Edward Lowassa,
pamoja na mawaziri, wabunge na viongozi mbalimbali nchini na nje ya
nchi.
Mazishi hayo yamelifanya jiji la Arusha kukumbwa na simanzi tangu
kiongozi huyo afariki Alhamisi iliyopota katika Hospitali ya Arusha
Lutheran Medical Center (ALMC) maarufu kama Seliani iliyoko jijini hapa
inayomilikiwa na kanisa hilo.
Rais Kikwete alisema kifo cha Laizer mbali ya kuacha pengo kubwa,
mchango wake ulikuwa bado unahitajika kuendeleza yale ambayo aliyaasisi
kwa maendeleo ya kanisa hilo.
“Mtu hakumbukwi kwa mali alizoacha bali kwa mema aliyoyatenda akiwa
duniani na hakika marehemu Askofu Laizer ni wa kukumbukwa kwani alikuwa
jasiri na tuseme kama alikuwa jabali la maendeleo la kanisa la KKKT,”
alisema Rais Kikwete.
Askofu Laizer alifariki kwenye hospitali hiyo baada ya kulazwa katika
vipindi tofauti kwa maradhi ya saratani ambapo kwa mujibu wa katiba
alipaswa kushikilia madaraka hayo hadi 2016.
Mkuu wa kanisa hilo nchini Dk. Alex Malasusa katika mahubiri yake
alimtaja marehemu kama shujaa wa imani, huku akiwasihi waombolezaji
kujiandaa na safari ya mwisho kwenda mbinguni na kamwe wasijione wote ni
wasafi.
Katika mazishi hayo maaskofu 20 toka dayosisi mbalimbali nchini na
wachungaji mbalimbali walishiriki ambapo mwili wake ulilala kanisani
hapo kuruhusu waombolezaji kutoa heshima za mwisho.
“Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe, akitoa salamu zake; awali alimwomba Katibu Mkuu wa KKKT, Israel
Kariongi, amuwie radhi ili aongee japo kwa dakika kumi tofauti na dakika
mbili zilizokuwa zimepangwa kwa kudai kuwa ni mara yake ya kwanza
katika hafla kama hiyo inayojumuisha Rais, marais wastaafu na waziri
mkuu mstaafu na mawaziri kwa wakati mmoja,” alisema Mbowe.
Alisema kuwa msiba ni somo kwamba viongozi wote wa kisiasa hutakiwa
kuacha itikadi zao na kujumuika pamoja na kwamba mara ya mwisho
alipomtembelea marehemu hospitalini, alimwagiza kusimamia ukweli na
kweli hiyo itamlinda.
Marehemu Askofu Laizer alizaliwa Machi 10, 1945 katika kijiji cha
Kitumbeine wilayani Longido, mkoa wa Arusha, na alipata elimu yake ya
msingi hadi darasa la nane Longido na kuhitimu mwaka 1965. Aliendelea na
masomo ya sekondari pamoja na masomo ya theolojia katika chuo cha
Makumira kabla ya kusimikwa rasmi kuwa askofu wa kwanza wa Dayosisi ya
Arusha ambapo sasa ni Dayosisi ya Kaskazini Kati.
No comments:
Post a Comment