ASKARI polisi mwenye namba G.68 PC Jafari Karume Mohamed (30),
amefariki dunia baada ya kurushiana risasi na watu wanaodhaniwa kuwa
majambazi wilayani Chunya mkoani hapa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki, aliwaambia
waandishi wa habari kuwa kifo hicho kilitokea jana katika hospitali ya
Wilaya ya Chunya.
Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni majambazi wanne wakiwa na
silaha aina ya SMG kuvamia kituo cha mafuta kilichopo Kijiji cha
Matundasi mali ya Samora Muyombe na kupora fedha sh milioni 2.2.
''Majambazi hao walitumia gari lenye namba za usajili T 227 BST aina
ya Toyota Corolla iliyokuwa ikiendeshwa na Shaban Msule (33) mkazi wa
Makambako mkoani Njombe,'' alisema.
Kamanda aliongeza kuwa, askari huyo aliyeuawa alikuwa doria na
wenzake, ndipo wakafuatilia tukio hilo na katika mapambano ya
kurushiana risasi, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi upande wa ubavu wa
kulia na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi.
Katika mapambano hayo, mtuhumiwa wa ujambazi, Msule aliuawa kwa
kupigwa risasi na gari lililotumika katika tukio hilo lilikamatwa na
maganda tisa ya risasi aina ya SMG/SAR na risasi sita ziliokotwa eneo
la tukio.
Kamanda Masaki ametoa wito kwa watuhumiwa hao waliotoroka
kujisalimisha wenyewe kabla hawajakamatwa kutokana na msako unaoendelea
chini ya Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa Mbeya, Robert Mayala.
No comments:
Post a Comment