Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema kuwa majeshi ya nchi yake
yatabakia nchini Mali kwa muda mrefu iwapo yatahitajika kuendelea
kupambana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu kaskazini mwa nchi
hiyo.
Akizungumza kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako, hapo jana (02.02.2013),
Rais Hollande alisema ugaidi umerudishwa nyuma, lakini bado
haujatokomezwa kabisa. Wakati majeshi ya Ufaransa na Mali yakiendelea na
jitihada za kuukomboa mji wa Kidal, ngome ya mwisho ya waasi
waliolitawala eneo la kaskazini mwa miezi 10 kabla ya majeshi ya
Ufaransa hayajaivamia nchi hiyo kijeshi, Rais Hollande amewaambia
wananchi wa Mali kwamba ni muda kwa Waafrika kuongoza operesheni za
kijeshi, lakini Ufaransa haitawatenga na kuwaacha peke yao.
Amesema Ufaransa itakuwa bega kwa bega na Mali kwa muda wote
unaohitajika hadi hapo Waafrika watakapoweza wenyewe kuongoza operesheni
za kijeshi. Akiwa mjini Timbuktu, alikopokewa kama shujaa, Rais
Hollande aliwashukuru wanajeshi wa Ufaransa na Mali kwa juhudi zao za
kuwaondoa waasi kaskazini mwa Mali, ingawa amekumbusha kuwa operesheni
hiyo ya kijeshi bado haijamalizika.
Rais wa Mali amshukuru Hollande
Rais wa mpito wa Mali, Diancounda Traore, amemshukuru Rais Hollande
kutokana na ufanisi wa wanajeshi wa Ufaransa, ambao amesema umelifanya
eneo la kaskazini kukombolewa na kuwa huru.
Mbali na Rais Traore kumshukuru Rais Hollande, wakaazi wa mji
huo pia wamemshukuru kiongozi huyo wa Ufaransa na kuahidi kumshukuru
milele ingawa wamemkumbusha kuwa amefanikiwa kuukata mti, lakini bado
ana jukumu la kuondoa kabisa mizizi ya mti huo.
Marais hao wawili walizuru pia katika msikiti wa Djingareybar mjini
Timbuktu uliojengwa kwa udongo miaka 700 iliyopita pamoja na maktaba ya
Ahmed Baba kwa ajili ya mambo ya kale.
Aidha, walipozuru makaburi mawili ya maimamu ambayo waasi hao
waliyaharibu mwezi Julai mwaka uliopita kwa madai kwamba wanaabudu
sanamu, Rais Hollande amewaambia maimamu wa msikiti huo kuna haja ya
kuuteketeza kabisa kwa sababu hakuna kitu kilichobakia. ''Tutayajenga
tena mheshimiwa rais,'', alisema Irina Bokova, mkuu wa Shirika la Umoja
wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Wakati rais huyo wa Ufaransa yuko Timbuktu, majeshi ya Ufaransa na Mali
yalipambana na waasi. Afisa mmoja wa jeshi la Mali ameyasema hayo na
kuongeza kuwa waasi waliitumia fursa hiyo kufanya mashambulizi yao,
wakitarajia kwamba wanajeshi wangelikuwa wameshughulika zaidi na
kuwasili kwa Rais Hollande.
Ufaransa na nia ya kukabidhi operesheni za kijeshi
Huku waasi wakiwa wamefurushwa kutoka miji yote mikubwa isipokuwa Kidal
uliopo kaskazini mashariki, Ufaransa ina nia ya kukabidhi operesheni za
kijeshi kwa karibu wanajeshi 8,000 wa Afrika ambao wanawasili taratibu
nchini Mali na walioidhinishwa na Umoja wa Mataifa.
Wanajeshi wa Mali
Lakini kuna wasiwasi kuwa Mali inahitaji msaada wa muda mrefu
na huku makundi ya haki za binaadamu yakiripoti mauji yaliyofanywa na
wanajeshi wa Mali pamoja na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu.
Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa wanajeshi wa Mali wamewauwa
kwa kuwapiga risasi watu wapatao 13 wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa waasi
wenye itikadi kali za Kiislamu katika mji wa Sevare na kuitupa miili yao
kwenye visima.
Baadhi ya waliokumbwa na mkasa huo kabla ya majeshi ya Ufaransa
hayaijavamia Mali kijeshi, ni watu wa jamii wa Kituareg na Kiarabu.
Kutokana na kuongezeka wasiwasi wa kuzuka mashambulizi zaidi, watu wa
jamii hizo wamekimbia katika eneo hilo la kaskazini.
Mzozo wa Mali umesababisha watu 377,000 kuyakimbia makaazi yao, wakiwemo
150,000 ambao wameomba hifadhi ya ukimbizi katika mipaka ya Mali.
Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Rais Hollande amewatolea wito wanajeshi wa Mali kuheshimu na kuzingatia
haki za binaadamu, wito ulioungwa mkono na Rais Traore ambaye pia
ameahidi kuongoza mchakato wa maridhiano ya kitaifa na kurejea msimamo
wake kwamba anataka kuitisha uchaguzi ifikapo Julai 31, mwaka huu.
Traore aipongeza timu ya mpira wa miguu ya Mali
Timu ya taifa ya soka ya Mali
Ama kwa upande mwingine, Rais wa mpito wa Mali, Diancounda
Traore ameipongeza timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Mali baada ya
kupata ushindi wa mabao matatu kwa moja ikiwa ni mikwaju ya penalti
dhidi ya Afrika Kusini katika michuano ya Kombe la Mataifa ya
Afrika-AFCON 2013, inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Timu hizo zililazimika kupigiana penalti baada ya mchezo kumalizika
zikiwa zimetoka sare ya kufungana bao moja kwa moja. Amesema ushindi wa
timu ya Mali kuingia nusu fainali, ambao ni ushindi wa kwanza tangu
mwaka 1972 ni hatua ambayo imeongeza thamani na ufahari wa Mali, licha
ya nchi hiyo kuwa katika mzozo. Amesema ushindi huo utaisaidia Mali
kurejea tena katika amani.
No comments:
Post a Comment