MAMA mzazi wa aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, marehemu
Steven Kanumba, Flora Mtagoa, amelalamikia kitendo cha mtu
aliyetengeneza na kusambaza kalenda zenye picha ya mtoto wake bila
idhini yake.
Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Flora alisema ni
bora yule aliyetoa kitabu, alifanya ustaarabu pamoja na Zamaradi Mketema
aliyetoa ‘CD’ iliyokwenda kwa jina la ‘Neno la Mwisho’ ambao walifuata
taratibu na ridhaa, kisha kumlipa fedha aliyotaka.
“Zamaradi na yule aliyechapa kitabu cha Kanumba, hawa walikuja
wakazungumza na mimi nikawatajia fedha niliyotaka wakanilipa bila
ubishi, lakini huyu mtu aliyefyatua kalenda za mwaka huu, yeye hana
ustaarabu, kwani amejifanyia kiholela tu kwa kutumia jina la mtoto wangu
bila ridhaa yangu na hajailipa familia chochote, hii si sawa,”
alilalamika Flora.
Aliviomba vyombo vya habari vimsaidie kumtafuta mhusika huyo kwa
sababu hata namba walizoziandika chini ya kalenda hizo zikipigwa
hazipatikani.
Aliongeza kuwa baada ya kifo cha mwanaye, wapo watu wengi waliofaidika
huku wengine wakitangaza kuwa wamevunja rekodi ya mauzo lakini bila
hata kwenda kuipa familia kiasi chochote cha fedha kama pole.
“Mwanangu, wapo wengi waliofaidika kibiashara na kifo cha Kanumba, pia
wapo wengine ambao walidiriki kutangaza hadharani kwamba wamevuka
malengo, inasikitisha sana,” alisema.Hivi sasa Flora anajipanga kuadhimisha mwaka mmoja tangu kijana wake
Steven Kanumba alipofariki dunia Aprili 7, mwaka jana nyumbani kwake
Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment