MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, ameponda hatua ya serikali kuunda tume ya kuchunguza
chanzo cha matokeo mabaya ya kidato cha nne, akisema kufanya hivyo bila
uwajibikaji ni matumizi mabaya ya rasilimali za walipa kodi.
Akitoa salaam baada ya kushiriki uzinduzi wa jengo la Chuo cha Walezi
wa Watoto cha Kumbukumbu ya Helen, katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Neema wilayani Hai, Mbowe alisema
mkakati huo ni wa kupunguza hasira ya umma dhidi ya serikali.
Alisema kuwa kutokana na ubovu wa mfumo wa elimu, kinachohitajika si
tume ya kuchunguza mambo yanayojulikana, bali kunahitajika hatua za
kisera, kibajeti, kitaasisi na kiuongozi.
Mbowe alifafanua kuwa masuala hayo serikali ya CCM haiko tayari
kuyafanyia kazi kwa sababu ya kupuuza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya
nchi.
Alisema kuwa kitendo cha wa Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa, na
viongozi waandamizi wenzake wizarani kuendelea kuingia ofisini huku
asilimia 90 ya wanafunzi wa sekondari wakiwa wamefeli vibaya ni aibu kwa
Waziri Mkuu na Rais.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisisitiza
kuwa hatua yoyote inayochukuliwa na serikali katika suala hilo inapaswa
kutanguliwa na uwajibikaji kwa watu waliopewa dhamana ya kusimamia
elimu ya watoto wa Tanzania.
“Ndugu zangu leo tunashuhuhudia tukio muhimu sana hapa Kalali,
kuanzishwa kwa chuo kitakachofundisha walimu au walezi wa watoto hawa
yatima walioko hapa ambao kweli ni watoto waliokosa fursa fulani katika
maisha yao.
Alisema kuwa wakati wanafikiria kuwatunza hao watoto yatima, ni vyema
wakaanza kutafakari kama taifa juu ya elimu ambayo wamewatia giza katika
upeo wa macho yao na maisha yao kwa kuwafelisha.
Mbowe alisema kuwa hana haja ya kupinga hatua ya Pinda kuunda tume,
lakini hatua yoyote itayochukuliwa na serikali bila kuendana na
uwajibikaji ni ghiliba kubwa kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment