SERIKALI imemuondoa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini
na kuagiza kufutwa kwa katiba mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
na badala yake itumike ile ya mwaka 2006.
Hatua hiyo, imekuja baada ya hivi karibuni kuibuka kwa utata juu ya
katiba mpya ya TFF, iliyopitishwa kwa njia ya waraka, wakati wa kuelekea
uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Februari 24 na
ule wa Bodi ya Ligi Februari 22, kabla ya kusitishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema
kuwa ameamua kumteua msajili mpya, baada ya aliyekuwepo kupitisha katiba
mpya ya TFF kinyume na utaratibu.
Alisema kuna mengi yalijitokeza ikiwemo baadhi ya wagombea kulalamikia
kuenguliwa, hivyo wizara iliamua kuliangalia hilo kwa uzito unaostahili
na kuamua kuchukua hatua stahiki.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
Mukangara alisema sheria Na.12 ya BMT na marekebisho yake Na.6 ya
mwaka 1971 pamoja na kanuni za BMT na kanuni za usajili Na. 442 mwaka
1999 zimekiukwa.
Alisema kuwa zipo taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa Shirikisho la
Soka la Kimataifa (FIFA) litakuja Tanzania, hivyo anamuelekeza Msajili
na anailekeza TFF kuitaarifu kuhusu maelekezo hayo ya kutumia katiba ya
mwaka 2006, na waambiwe hali halisi iliyojitokeza.
Mukangara alisema anaielekeza TFF iitishe mkutano mkuu kwa msingi wa
katiba yao ya mwaka 2006 na kanuni za BMT na wafanye uchaguzi kwa mujibu
wa katiba hiyo kwa kuzingatia sheria za BMT.
Alisema kanuni ya BMT Na.11(1), inaeleza wazi utaratibu wa marekebisho
ya katiba haikufuatwa, kwani kimsingi, TFF ilitakiwa ijaze fomu Namba
6,7,8 na 9 kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT.
Mukangara alisema kimsingi upo utaratibu wa kurekebisha katiba za
vyama vya michezo, kwa mujibu Sheria ya Baraza la Michezo iliyotungwa na
Bunge, na kanuni zake ziko wazi na ni rahisi kuzielewa.
“Sasa TFF hawakufuata taratibu kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT.
“Baada ya kupitia taarifa mbalimbali za BMT, nimejiridhisha kuwa
katiba itakayotumika ni ile ya mwaka 2006, ikiwa ni pamoja na TFF
kuitisha mkutano mkuu na kutumia katiba ile ile ya mwaka 2006,” alisema
Mukangara.
Alisema kwa mamlaka aliyonayo, anaagiza msajili awajulishe TFF, kufuta
matumizi ya katiba ya mwaka 2012 na watumie ya mwaka 2006 na barua
ilifikie shirikisho hilo kabla ya saa 7 mchana, jana.
Waziri huyo, alitoa maagizo kwa msajili kufuata taratibu za usajili kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT.
Alibainisha kuwa kuna taarifa ya uwezekano wa FIFA, ikachukua hatua
kali juu ya serikali kuingilia, kitu ambacho amedai si kweli.
Mukangara aliongeza kuwa kila nchi ina Katiba yake, hivyo si kweli kama FIFA wanaweza kuifuta Katiba ya nchi.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kuhusu uamuzi wa
serikali, alisema ni mapema mno kwao kusema lolote hadi pale
watakapopata rasmi taarifa hiyo.
“Hatuwezi kusema lolote, kwani hatujapata taarifa rasmi ya serikali
tujue kama ni maoni, ushauri au agizo. Tukishajua ni kitu gani, TFF kama
taasisi ndipo kwa kutumia vyombo vyake vya maamuzi, itatoa uamuzi na
msimamo wake,” alisema Osiah.
Hata hivyo akaongeza kuwa kama ni agizo hakuna tafsiri nyingine ya
kilichofanyika, isipokuwa serikali kuingilia masuala ya uendeshaji wa
soka, jambo ambalo limekuwa likipingwa na FIFA.
No comments:
Post a Comment