Timu za taifa za Nigeria 'Super Eagles' na Burkina Faso zimefanikiwa
kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika
inayoendelea kurindima nchini Afrika Kusini. Nigeria imefanikiwa kutinga
hatua ya nusu fainali baada ya kuichabanga Ivory Coast kwa mabao 2-1.
Ilikuwa Nigeria iliyoanza kuzifumania nyavu za Ivory Coast 'The
Elephants' katika dakika ya 43 kwa bao lililofungwa na mshambuliaji
Emanuel Emenike
Kipindi cha pili kilipoanza Ivory Coast
walicharuka na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha lililopachikwa na
mchezaji wa kiungo Cheikh Tiote katika dakika ya 50. Hata hivyo, Sunday
Mba aliifanikiwa kumuangusha 'mnyama' na kumchinjia baharini katika
dakika ya 78.
Nigeria itakwaruzana na Mali katika hatua ya nusu fainali siku ya Jumatano.
Mali ilifanikiwa kupata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya
kuwatoa wenyeji, Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti baada muda wa
kawaida na wa nyongeza kwa timu hizo kufungana bao 1-1. Kwenye mikwaju
ya penalti, Mali ilipachika mabao 3 na Afrika Kusini bao 1. Hivyo Mali
ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mtanange mwengine wa robo fainali, Burkina Faso imefanikiwa
kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibwaga Togo kwenye mechi ngumu
iliyotawaliwa na ubabe na wachezaji kurushiana madaruga. Kwenye mchezo
huo, Burkina Faso imeweza kuinyoa Togo kwa bao 1-0.
Hadi dakika ya 90 ya
mchezo hakuna timu iliyoweza kutoboa nyavu za timu pinzani, na muda wa
nyongeza wa dakika 30 ziliweza kuamua nani anasonga mbele. Jonathan
Pitroipa aliipatia Burkina Faso bao pekee katika dakika ya 105 ya
mchezo. Wachezaji sita wa Togo na wawili wa Burkina Faso walionyeshwa
kadi za njano kwa kucheza rafu.
Kwa matokeo hayo, Burkina Faso itakwaruzana na Ghana siku ya Jumatano kwenye mchezo wa nusu fainali.Ghana walifanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuifunga Cape Verde mabao 2-0 kwenye mchezo wa robo fainali.
No comments:
Post a Comment