WIMBI la wizi wa fedha kwenye mitandao ya benki kupitia njia ya
mashine za kuchukulia fedha (ATM), umewatia hasara wateja wengi wa
benki ambao zaidi ya sh milioni 20 zinadaiwa kuchotwa kwa nyakati
tofauti na watu wanne wanaomiliki kadi zipatazo 150.
Uchunguzi uliofanywa umegundua kuwepo kwa
mtandao wa wizi kwa njia ya ATM unaotumiwa na watu wanaojifanya kuwa ni
madalali wa fedha wanaowalaghai watumishi wa serikali.
Madalali hao wanadaiwa kuwakopesha watumishi hao wa serikali kwa
sharti kwamba wawapatie kadi zao za kuchukulia fedha benki kama dhamana.
Uchunguzi umebaini kuwa, mtindo huo umeenea katika maeneo kadhaa
mkoani Mbeya na hasa ukiwalenga watumishi wa serikali ambao kutokana na
hali ngumu ya kifedha, wamejikuta wakiingia kwenye mtego huo na kuamua
kutoa kadi zao za ATM ili waweze kupata mikopo.
Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa waathiriwa wa wizi huo
wa mtandao, unasema kuwa wapo madalali ambao wanawafuata watumishi wa
serikali kwa lengo la kuwakopesha fedha kwa masharti kwamba watoe kadi
zao za ATM na namba za siri kama dhamana.
“Mtandao wa kuchukua fedha kutoka kwa watumishi wa umma umeenea sana,
haukuanza leo, wapo watu wanakopesha fedha kwa sharti la kutoa kadi ya
ATM na namba yako ya siri ili mshahara wako unapoingia, wao wanakwenda
kuchukua fedha zao walizokopesha na riba,” alisema mtumishi mmoja wa
serikali jijini Mbeya.
Wakati hali ikiwa hivyo, habari kutoka Wilaya ya Rungwe zinadai kuwa
kiasi kikubwa cha fedha kimechukuliwa benki na watu wanaomiliki kadi za
ATM zaidi ya 120, na kwamba tayari Jeshi la Polisi linawashikilia watu
hao ambao wamekutwa na idadi hiyo ya kadi zisizokuwa zao.
Habari zaidi zinasema kuwa, mtandao wa madalali hao wa fedha umekuwa
mkubwa, na kwamba watu hawaibiwi kwani wametoa kadi zao wenyewe baada ya
kukubali kukopeshwa.
“Ndugu mwandishi tumefikia uamuzi huu kutokana na hali ngumu ya
maisha, watoto wanatakiwa walipiwe ada, tunahitaji mbolea kwa ajili ya
kilimo na gharama za maisha zipo juu, tutafanyaje? Ndiyo maana
tumejikuta tukitoa kadi zetu za ATM ili tutatue matatizo yetu, kama wapo
matapeli hilo sijui, ila wengi tumeingia kwenye mtego huo,” alisema
mama mmoja aliyejitaja kuwa ni muuguzi.
Meneja mmoja wa benki ambaye hakutaka jina lake liandikwe wala benki
anayofanyia kazi, alisema wizi kwa njia ya ATM ni tatizo sugu kwa wateja
wao, kwani wamekuwa wakipokea malalamiko kila siku kuwa fedha zao
zinaibwa bila wao kujua.
Alisema hana taarifa kama kuna wateja wanaotoa namba zao za siri na kadi zao kwa madalali wa fedha.
“Kinachonishangaza benki yetu inakopesha, sasa huu mtindo uliozuka
kati ya wateja na madalali wa nje unatia shaka usalama wa fedha kwenye
benki zetu, inabidi hatua kali zichukuliwe kwa wateja wanaoruhusu watu
wengine wawachukulie fedha, hilo ni kosa la jinai kufanywa na wateja
wasiokuwa waaminifu,” alisema meneja huyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alipohojiwa
alisema kuwa amepokea taarifa za kuwepo kwa tukio hilo, hasa Wilaya ya
Rungwe na kwamba tayari anasubiri taarifa kamili kutoka kwa Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Mbeya (RCO) ili atoe taarifa
kamili leo.
No comments:
Post a Comment