MGOGORO ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba
Mjini, unazidi kuchukua sura mpya baada ya madiwani wake tisa kuungana
na wenzao wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) na wawili wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukwamisha kikao cha Baraza la
Madiwani kilichokuwa kiketi jana kujadili bajeti ya 2014/2014.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya madiwani 10 wa Halmashauri ya
Mji wa Bukoba akiwemo Mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagesheki
kutukanwa matusi ya nguoni kupitia vipeperushi vilivyosambazwa mjini
humo na watu wasiojulikana.
Madiwani waliotukanwa matusi hayo mazito ni nane wa CCM na wawili wa
CUF waliosaini hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha
kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani ili kumng’oa Meya Anatory Amani
anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Halmashauri hiyo ina madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na
17 wa CCM. Ili kikao cha baraza kiweze kuendelea ni lazima akidi ya
mahudhurio iwe na nusu ya wajumbe jambo ambalo lilishindikana jana.
Wakizungumza kutoka mjini Bukoba, baadhi ya
madiwani walisema kuwa Meya Amani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya
Kagondo, alipata wakati mgumu hadi kulazimika kukiahirisha kikao hicho.
Kwamba muda wa kuanza kikao ulipowadia, ukumbini walikuwemo wajumbe
11, yaani madiwani nane wa CCM, wawili wa CHADEMA na mmoja wa CUF, jambo
lililomlazimu meya huyo kuwapigia simu baadhi ya wale ambao walikuwa
hawajafika na kuwashawishi bila mafanikio.
“Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Zipora Pangani naye aliingilia kati
kumsaidia meya kiasi cha kufikia hatua ya kuwapigia simu madiwani hao,
kila mmoja akimbembeleza ataje mahali alipo ili amtumie gari imchukue au
kitabu cha mahudhurio asaini huko aliko, lakini ilishindikana,” alisema
mmoja wa madiwani.
Habari zaidi zinasema kuwa, Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera naye
aliingilia kati kwa
kumwagiza katibu wa wilaya awatafute madiwani wa
chama hicho ambao hawakuwa ukumbini, lakini haikuwezekana kwani simu zao
zilikuwa zimefungwa.
Baada ya kuona hali inakuwa tete, Meya Amani alikiahirisha kikao kwa
muda hadi saa 6:30 mchana ingawa hali iliendelea kubakia vile vile, na
hivyo ukafikia uamuzi wa kusitisha baraza hilo hadi Machi 1 na 2 mwaka
huu.
Akiahirisha kikao hicho, Meya Amani kwa hasira alisema kuwa madiwani
hao waliokwepa wanapaswa kupigwa mawe na kulaaniwa kwa kukwamisha
maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo, tarehe hizo zilizopangwa kufanyika baraza hilo zimezua
utata kwani zilishapangiwa shughuli nyingine ya vikao vya kujadili
utekelezaji wa bajeti ya robo mwaka ya pili ya 2012/2013.
Ni dhahiri kuwa mgogoro huo unazidi kukimega chama kwani Meya Amani
kwa upande mwingine amepuuza maagizo ya Makamu Mwenyekiti CCM Taifa,
Philip Mangula kwa kuamua kufungua kesi mahakamani kupinga kujadiliwa na
kung’olewa na madiwani.
Mangula ambaye alilazimika kufika mjini Bukoba mwezi uliopita ili
kunusuru mtafaruku huo, aliagiza madiwani nane wa CCM waliokuwa
wamesaini hati hiyo, waondoe tuhuma hizo na kuzipeleka kwenye chama ili
zipatiwe ufumbuzi.
Madiwani waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya
huyo mbali na Kagasheki ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Kata ya
Buhende) na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Manispaa ya Bukoba.
Wengine ni Richard Gasper (Miembeni), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo),
Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe) na Mulubi
Kichwabuta (Viti Maalumu) na wale wa CUF ni Ibrahim Mabruk (Bilele) na
Rabia Badru wa Viti Maalumu.
Taarifa kutoka mjini Bukoba zilisema kuwa madiwani hao nane wa CCM,
jana waliandika barua ya malalamiko kwenda kwa katibu wa chama hicho
wilaya na nakala zake kwa Mwenyekiti wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa na Mangula.
Juzi, madiwani nane wa CCM walikabidhi barua kwa Katibu wa Wilaya
wakipinga kushiriki vikao vyote vitakavyoongozwa na Meya Amani
wakimtuhumu kuwa ndiye alihusika kusambaza vipeperushi vya kuwakashifu.
Katika vipeperushi hivyo, madiwani hao kila mmoja alitajwa kwa jina
lake, kata na orodha ya tuhuma zake huku wengine wakidaiwa kulaghaiwa
kwa fedha na mmoja wa viti maalumu akidhalilishwa kwa tuhuma za ngono.
Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na
madiwani wenzake kadhaa wa CCM, waliwasilisha barua zao kwa mkurugenzi
ili kuondoa tuhuma zao kwa muda asubuhi ya Januari 23 mwaka huu, lakini
mchana wa siku hiyo Meya Amani akafungua kesi ya kupinga asijadiliwe.
Mangula aliwataka madiwani hao kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro
huo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe ingawa mkuu huyo
pamoja na Pangani, Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wanadaiwa kumkingia
kifua Amani.
Madiwani hao wanapinga mikataba ya miradi mikubwa miwili ya uuzwaji wa
viwanja zaidi ya 5,000 na ujenzi wa soko la kisasa wakidai imasainiwa
kifisadi kwa siri na Meya Amani.
No comments:
Post a Comment