ASKARI Polisi PC Yohana mwenye namba 7771 amemuua kwa kumpiga
risasi mwendesha bodaboda, Makisio Ngonyani (27), kisha naye akauawa na
watu wenye hasira kwa kutumia mawe na mbao.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana katika eneo la Ngwinde wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, lilitokea majira ya saa 8
mchana jana ambapo PC Yohana na mwenzake PC Venance Kamugisha wa kituo
kikuu cha polisi cha wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, walikuwa katika
doria ya kawaida.
Walipofika katika Kijiji cha Litola na kupata chakula cha mchana
kwenye moja ya migahawa iliyopo hapo, walianza kazi ya doria ya kawaida
ambapo alitokea mwendesha bodaboda huyo akiwa amebeba abiria wawili
kinyume na sheria ya usalama barabarani na walipomsimamisha, hakutii
amri hiyo huku kundi jingine la waendesha bodaboda likiwazuia askari hao
kufanya kazi yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, hali hiyo ilimfanya PC Yohana kufyatua
risasi iliyompata mmoja wa abiria kwenye kidole cha mkono na kisha
kupitiliza na kumpiga Ngonyani kichwani na kusababisha kifo chake papo
hapo.
Baada ya tukio hilo, askari hao walikimbia na pikipiki waliyokuwa
nayo, huku wakifukuzwa na kundi la waendesha bodaboda wengine hadi
katika Kijiji cha Ngwinde ambapo waliwazingira na kumpiga kwa mawe PC
Yohana na kumsababishia kifo huku wakimjeruhi PC Kamugisha ambaye
alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Ruvuma, Deusdedit Nsimeki aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu akiwa
eneo la tukio kwamba askari huyo aliuawa kwa kutumia mawe na mbao.
No comments:
Post a Comment