MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) taifa, kupitia Mkoa wa Arusha, Benson Mollel (26) amekutwa
amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business, iliyopo Mtaa
wa Jacaranda katikati ya Jiji la Arusha.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mollel alikutwa
akiwa amekufa jana mchana na kwamba tukio hilo limezua hofu kwa wakazi
wa Jiji la Arusha, huku wakijiuliza chanzo cha kifo chake.
Kifo cha mwanasiasa huyo mchanga ambaye pia
alikuwa ni mfanyabiashara wa madini mkoani hapa, kimezusha maswali mengi
wakati wengine wakihusisha tukio hilo na masuala ya kisiasa na upande
mwingine wakidai ni masuala la kibiashara.
Hisia hizo zinatokana na ukweli kwamba Arusha ni
jiji lenye hekaheka za kisiasa hasa ndani ya CCM ambapo Mollel alikuwa
mmoja wa vinara wake.
Polisi waliwasili hotelini hapo saa 8.00 mchana na
kuupakia mwili wa marehemu kwenye gari na kisha kuupeleka Hospitali ya
Mount Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya wa Arusha (OCD), Gilles
Muruta akizungumza katika eneo la tukio alisema: “Tunachunguza tukio
hili ambalo ni la ghafla.”
Akizungumzia kifo hicho, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela
alisema: "Tumepokea kwa masikitiko kifo cha Mollel japokuwa sifahamu
nini hasa kimejiri huko."
"Kuna rafiki yake alinipigia simu kuniarifu kuhusu
kifo hicho na nikawaambia kama UVCCM Taifa tupate maelezo kamili na
tujue nini cha kufanya. Iwapo familia itakuwa na mipango yoyote
watutaarifu," alisema Shigela.
Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wa madini
mkoani Arusha walionekana nje ya hoteli hiyo baada ya taarifa za kifo
hicho kusambaa na wengine walishindwa kujizuia kisha kuangua vilio.
Miongoni mwao ni kada wa Chadema, James ole Millya
na diwani wa CCM Kata ya Mlangarini, Mathias Manga. Katibu Mwenezi wa
CCM wa Mkoa wa Arusha, Isaack Kadogoo ambaye pia alifika eneo hilo
alisema kwamba wamepokea taarifa za tukio hilo kwa mshtuko mkubwa.
Uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kulizungumzia kwa madai kwamba limefikishwa katika vyombo vya usalama.
Hata hivy, kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani
ya hoteli hiyo vilidai marehemu aliwasili usiku, juzi Jumamosi hotelini
hapo akiongozana na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Nancy na
kuchukua chumba namba 208.
Mmoja wa walinzi hotelini hapo aliyetembulika kwa jina la Obeid
Mollel kutoka Kampuni ya Ulinzi ya Victoria Support Services, alisimulia
kuwa marehemu aliingia na mwanamke huyo na kisha kuondoka ghafla kabla
ya kurejea tena wakiwa wote usiku.
Alisema kuwa wakati wakiwa hotelini hapo marehemu
aliomba kuegesha gari lake jipya aina ya Mark II Grande ambalo
halijasajiliwa na kwamba alipokubaliwa alifanya hivyo kisha akaenda
chumbani. Ilibainika kuwa mwanamke huyo aliondoka jana asubuhi.
Taarifa zaidi
Mmoja wa wahudumu hotelini hapo (jina lake
limehifadhiwa), alisema kuwa mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la
Mariam aliwasili hotelini hapo saa 5.00 asubuhi na kuomba kupelekwa moja
kwa moja chumba alichokuwapo marehemu.
Mhudumu huyo alisema wakati mwanamke huyo akiomba
kupelekwa chumbani, marehemu naye alipiga simu mapokezi akiomba mwanamke
huyo apelekwe chumbani kwake, agizo ambalo walilitekeleza.
Kwa mujibu wa mhudumu, baadaye kama saa 6.00 mchana walimwona mwanamke huyo akitoka nje ya hoteli hiyo na kuondoka.
Alisema kwamba baadaye waliamua kupiga simu ya chumba alichofia
marehemu ili kujua endapo ataendelea kupanga kwani muda wa kawaida
ulikuwa umemalizika lakini simu hiyo ilikuwa ikiita bila majibu.
Mmoja wa wahudumu ambaye alikuwa akifahamiana na
marehemu, aliamua kumpigia kupitia simu yake ya mkononi lakini nayo
haikupokewa.
Mhudumu huyo aliamua kupanda ngazi kwenda chumbani
kwa marehemu na katika hali isiyo ya kawaida alikuta mlango ukiwa wazi
na marehemu akiwa amelala.
"Nilijaribu kumwamsha, lakini hakuamka na ndipo
alipotoa taarifa kwa uongozi wa hoteli na baadaye waliviarifu vyombo vya
usalama.
Chanzo cha kifo hiki kinakanganya maana kama kweli
ni mauaji basi yamefanyika kwa ustadi mkubwa,” alisema mhudumu huyo na
kuongeza:
“Unajua vyumba vyote vya huko juu ghorofani
ukifunga mlango tu huku chini sisi mapokezi tunasikia, sasa cha ajabu
mlango tumeukuta wazi. Hapa kuna maswali mengi," alieleza mhudumu huyo.CHANZO NI MWANANCHI
No comments:
Post a Comment