WAKATI hali ya Shirika la Ugavi Tanzania (TANESCO) ni mbaya
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Eliakimu Maswi, wanatajwa kuwa chanzo cha kulidhoofisha
kiuchumi shirika hilo, Tanzania Daima Jumatano, limedokezwa.
Vigogo hao wanadaiwa kuingilia shughuli za kiutendaji za shirika hilo kisiasa na kwa maslahi ya watu binafsi.
Vyanzo vya habari toka serikalini na TANESCO vinasema Muhongo na Maswi
wamekuwa wakiliendesha shirika hilo kama taasisi binafsi kinyume na
taratibu, jambo ambalo limesababisha hasara ya mabilioni ya shilingi kwa
shirika hilo tangu waingie madarakani.
Duru za kisiasa kutoka ndani ya shirika hilo, zinasema kuwa kumekuwa
na msigano wa kimaamuzi kati ya shirika hilo na Wizara ya Nishati na
Madini.
Inaelezwa kuwa wakati Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, Felchesmi
Mramba, akianzisha mchakato wa kuomba maoni ya wadau kupandisha bei,
Waziri Muhongo aliibuka kupinga mawazo ya kupandisha bei kwa maelezo
kuwa shirika lina pesa nyingi na serikali inalipatia ruzuku.
Mramba katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi, alisema kuwa
kwa hali ilivyo sasa, hata kama TANESCO ikiamua kutolipa mishahara wala
isifanye matengenezo ya mitambo, isinunue vifaa vya kuunganishia wateja,
au isiingie gharama nyingine zozote, bado ingepata hasara ya karibu sh
bilioni 90 kila mwezi, hivyo lazima bei ya nishati hiyo ipande ili
liweze kujiendesha.
Taarifa zaidi zinasema, menejimenti ya TANESCO haina mamlaka ya
kuendesha kitaalamu shughuli zake isipokuwa Maswi na Muhongo ambao
hawana sifa za utaalamu wa kuendesha shirika, huingilia utendaji.
“Maswi na Muhongo wamekuwa wakiingilia utendaji wa kila siku wa
TANESCO kwa sababu za kisiasa na sasa shirika hilo linaelekea kufilisika
kabisa kwani kwa sasa linatumia sh bilioni 5.4 kwa siku huku
likikusanya sh bilioni 2.3 tu, hali hiyo imetokana na maamuzi ya
kisaiasa yanayofanywa na viongozi hao,” alisema mtoa habari wetu.
Habari kutoka ndani ya TANESCO, zinasema kuwa Maswi na Muhongo
hawataki bei ya umeme ipande kwani wamekuwa wakisema serikali ndiyo
yenye shirika, menejimenti ya
TANESCO ni chombo cha kuelekezwa namna ya
kuiendesha tu.
Hivi majuzi, baada ya TANESCO kutaka kupandisha bei ya umeme Katibu
Mkuu Maswi aliingilia kati kumshauri Mkurugenzi wa Ewura Haruna Masebu
kuwa asikubali uamuzi wa TANESCO kwani ungeiaibisha serikali na
walipofanikiwa Maswi alinukuliwa katika andiko moja akimwandikia Masebu
kumpongeza:
“Bwana Masebu, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa
uungwana wako na kuamua kazi kwa kuilinda heshima ya serikali yetu.
Heshima haina duka. Nakushukuru sana na naomba tuendelee kuisaidia
serikali yetu pamoja na matatizo yaliyo mbele yetu.
Kwa aina hii ya
kushirikiana tutafika tu wala haina gogoro”
Wiki hii vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kuwa nchi iko
hatarini kuingia gizani wakati wowote kutokana na hali ya uzalishaji
umeme kuwa tete TANESCO.
Inaelezwa kuwa hali ya shirika kifedha ni mbaya licha ya serikali
kukwepa kukiri uwepo kwa mgawo ikihofia kubanwa kwa ahadi yake kuwa
mgawo ungelikuwa historia.
Julai 28 mwaka jana, wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara
ya Nishati na Madini, Waziri Muhongo na Naibu wake, George Simbachawene,
walilihakikishia Bunge kuwa mgawo wa umeme ungelikuwa historia.
Lakini kwa takriban wiki nzima sasa, umeme umekuwa ukikatika hovyo kwa
muda mrefu katika maeneo mengi nchini huku TANESCO ikitoa sababu za
kawaida kuwa hali hiyo inatokana na matengenezo madogo kwenye
miundombinu yake.
Habari zaidi za uchunguzi toka ndani ya TANESCO zinasema, hata mikopo
ambayo shirika linapata sasa ni kwa ajili ya kulipa madeni tu wala sio
kwa ajili ya kusaidia shirika hilo lisifilisike.
Ofisa habari wa TANESCO Badra Masudi alipoulizwa kuhusu hali hiyo,
alijibu kwa kifupi kuwa mchanganuo wa pesa za TANESCO uko wazi.
Waziri Muhongo alipoulizwa kupitia simu yake ya mkononi kuhusu suala hilo, alijibu kwa kifupi tu kwamba yuko kwenye mkutano.
Baadaye alipoandikiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi, hakuweza kujibu.
Ujumbe alioandikiwa na gazeti hili ulisomeka hivi: “Mheshimiwa Waziri,
jana Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO amesema shirika linaendeshwa kwa
hasara na wewe ulisema wanakusanya pesa nyingi, sana, taarifa ipi ni
sahihi? Pia tumepata taarifa kuwa unaiendesha TANESCO kisiasa; hufuati
ushauri wa wataalamu nini maoni yako?”
Waziri alijibu tena kwa kifupi kwamba yuko kwenye mkutano. Jioni alipopigiwa simu, hakuweza kupokea.
Tanzania Daima pia ilimuandikia ujumbe wa simu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini: “Mheshimiwa Maswi, unatuhumiwa kuingilia utendaji
wa kila siku wa TANESCO, je ni kweli? Au una taarifa zozote kuhusu
hili?” Katibu Mkuu hakujibu ujumbe wala kupokea simu.
CHANZO CHA HABARI NI TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment