CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kiko katika
hatua za mwisho za kuandaa utaratibu wa kufanya maandamano ya amani kwa
ajili ya kumng’oa madarakani Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa, na Naibu wake, Philipo Mulugo.

CHADEMA imeeleza kuwa maandamano hayo ni ya amani na lengo lake hasa ni kuinusuru elimu ambayo iko kaburini.
Akizungumza kwa njia ya simu, jana, Ofisa Habari wa Chama hicho,
Tumaini Makene, alisema kuwa maandalizi makubwa wameshayakamilisha na
wanachomalizia ni taratibu za mwisho na kueleza kuwa yatafanyika katika
kanda za chama hicho.
Akizitaja kanda hizo kuwa ni Kanda ya Ziwa katika mkoa wa Mwanza na
yatahusisha mikoa yote iliyo karibu na mkoa huo, Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini itakayohusisha mkoa wa Mbeya na mingine yote iliyo karibu.
Kanda nyingine ni ya Mashariki ambayo itahusisha jiji la Dar es salaam
na mikoa iliyo jirani na mkoa huo na Kanda ya Kaskazini itakayohusisha
mikoa ya Arusha, Manyara na mingine iliyo ndani ya kanda hiyo.
Makene alisema kuwa maandamano hayo yatakuwa ya kwanza na ya
kihistoria ambayo serikali haijawahi kuyashuhudia kwani yatahusisha
wananchi wote.
“Maandamano hayo yatahusisha wananchi wote, madereva wa bodaboda,
daladala, bajaji, mama lishe, wanafunzi waliofeli na hata wale ambao
hawajafeli, walimu na watu wote yaani kwa ufupi tusiite maandamano bali
ni mgomo wa wananchi,” alisema Makene.
Alieleza kuwa kufeli mtihani kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa
asilimia 94 si jambo dogo na ndiyo maana CHADEMA imepanga kuhakikisha
elimu inapanda daraja kwa kuwaondoa watu wanaokwazisha jitihada za
elimu.
“Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe aliwapa siku 14 wawe wamejiuzulu
lakini maadamu wamekataa kufanya hivyo sasa ni mgomo wa wananchi ili
kuhakikisha tunawaondoa madarakani,” alisema Makene.
Wameanza maandalizi ya maandamano hayo na watawatangazia wananchi siku husika.
“Baada ya kutoa maamuzi ya maana wao wanaanza kuunda tume ya ajabu na
wengine kukaa tu maofisini, tuko ‘seriuous’ katika hili na lazima
lifanyike,” alieleza Makene.
Nayo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imejitetea kuwa haipaswi
kushutumiwa yenyewe peke yake katika hilo kwani suala la elimu
linasimamiwa na wizara mbili.
Chanzo chetu cha ndani ambacho hakikutaka kutajwa jina kilieleza kuwa
wadau, wanasiasa na wananchi wamekuwa wakiing’ang’ania wizara hiyo pekee
ikiwemo kuwataka mawaziri wake kujiuzulu na kusahau kuwa suala la elimu
pia linasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi).
Chanzo hicho kilieleza kuwa mambo ya elimu yanahusisha wizara mbili
ndio maana wakati mwingine inakuwa ngumu kutolewa uamuzi na kuishauri
serikali kuamua moja katika suala la elimu ili libaki katika wizara moja
ili ufumbuzi upatikane.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP, Charles Kenyela,
alikiri kupokea barua ya taarifa ya maandamano ya amani kutoka CHADEMA.
“Nimepokea barua ya CHADEMA kuhusiana na maandamano juzi saa 9: 20
alasiri na tunajiandaa kutoa majibu na kuona namna ya kushughulikia
suala lao, lazima kufanya mawasiliano na kuona namna ya kukabiliana na
jambo hilo,” alisema Kenyela.
Awali Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, aliwapa siku 14
mawaziri hao kuachia nyadhifa zao jambo ambalo wamelikaidi na kubaki
madarakani.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa
ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini
kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na
kuandika.
Mbowe alisema hilo ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke
ndani ya wiki mbili, vinginevyo CHADEMA ingeliitisha maandamano makubwa
nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.
No comments:
Post a Comment